MOROGORO.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wahariri wa vyombo vya habari wahakikishe wanazingatia weledi na maadili katika uandishi wa habari ili umma uweze kupata habari zenye ubora.
Ametoa wito huo leo Mei 20, 2021 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 10 wa Jukwaa la Wahariri na kongamano la kitaaluma, Mkoani Morogoro
Amesema kuwa utendaji unaozingatia weledi ni chachu ya kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari na wamiliki wake.
“kaulimbiu yenu ya Vyombo vya Habari na Maendeleo inahamasisha uandishi wa uwajibikaji. Vyombo vya habari vinapaswa kutambua katika kila habari vinayoiandika kuwa nyuma yake kuna masilahi ya taifa. Visipofanya hivyo, upotoshaji unaweza kuigawa nchi yetu, kuhatarisha amani na mshikamano wetu”.
Aidha Waziri Mkuu ameviasa vyombo vyote vya habari nchini kuhakikisha vinatanguliza Uzalendo, Utaifa na Maslai ya Nchi katika kufanya kazi “Mjenga Nchi ni Mwananchi. Hakuna mwingine zaidi yenu wa kulisemea Taifa letu”
Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayewakwaza mwandishi wa habari wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Niwahakikishie kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yake na kwamba Serikali itaendelea kuimarisha misingi ya habari nchini. Kwa upande wenu wanahabari zingatieni sheria za nchi, msitumie vibaya kalamu zenu kuwachafua watu kwa chuki binafsi”.
Waziri Mkuu pia ameziagiza Wizara na Idara zote za Serikali ambazo hazijalipia matangazo zifanye hivyo mara moja ili kuviwezesha vyombo hivyo kujiendesha.
“Ikiwa tangazo limefuata utaratibu kuanzia upatikanaji wake hadi kuchapishwa linapaswa kulipiwa mara moja. Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nataka muangalie tatizo liko wapi na lipatiwe ufumbuzi”
Kadhalika Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kukamilisha mchakato wa kuundwa kwa Bodi ya Ithibati ya Habari itakalofanya kazi ya kusimamia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari ili kuwezesha uundwaji wa Baraza Huru la Habari.