Home LOCAL UCSAF YAWATAKA WADAU KUCHANGAMKIA FURSA ZINAZOTOLEWA NA MFUKO HUO.

UCSAF YAWATAKA WADAU KUCHANGAMKIA FURSA ZINAZOTOLEWA NA MFUKO HUO.

 


Na: Celina Mwakabwale- UCSAF

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umetoa wito kwa wadau wa Mawasiliano nchini wakiwemo wamiliki wa redio hasa radio jamii, runinga na huduma za waya (cable tv) kuchagamkia fursa zinazotolewa na Mfuko huo ili kuboresha usikivu wa vyombo vyao kwa lengo la kuwezesha watanzania wote kupata huduma bora za mawasiliano katika maeneo yao.

Hayo yameelezwa na Mhandisi Richard Sotery kutoka UCSAF katika mkutano wa siku moja kati ya taasisi hiyo na wadau wa mawasiliano kanda ya kati uliofanyika Mkoani Tabora, ukiwa na wadau kutoka mikoa ya Tabora, Kigoma na Singida.

Mhandisi Sotery ameongeza kuwa ni muhimu kwa watoa huduma za mawasiliano kuelewa malengo ya kuanzishwa Mfuko huo ili kutambua fursa zilizopo ikiwemo ruzuku ambayo hutolewa ili kusaidia kufikishwa kwa huduma za mawasiliano vijijini, kuboresha usikivu wa matangazo ya redio na runinga kwenye maeneo yenye usikivu hafifu na maeneo ya mipakani.

“Usikivu wa redio na mawasiliano ya simu bado ni changamoto katika maeneo mengi hapa nchini, natoa wito kwa watoa huduma za mawasiliano ikiwemo wamiliki wa redio kushirikiana na mfuko ili kwa pamoja tuhakikishe kuwa kila mtanzania anapata huduma hii muhimu kutoka kwa vyombo vya habari vya hapa nchini”. Alisema Mhandisi huyo.

Kwa upande wake Mhandisi Shirikisho Mpunji kutoka UCSAF akiwasilisha mada amesema, lengo lingine la kufanyika kwa mkutano huo ni kuwafahamisha wadau kuhusu haki na wajibu wao kwa Mfuko pamoja na kujenga mahusiano bora yatakayoiwezesha taasisi hiyo kufanya kazi kwa ukaribu na kwa kushirikiana na watoa huduma za mawasiliano.

Naye Afisa Sheria wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Kati, Joseph Kavishe amewataka wadau hao wa mawasiliano kutumia vema fursa zinazotolewa na UCSAF huku akiwataka kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Mamlaka hiyo katika kusambaza maudhui kwa watanzania.

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, ulianzishwa na Serikali kwa lengo la kupeleka na kufanikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi waishio katika maeneo machache ya mijini na maeneo ya vijijini yasiyo na mvuto wa kibiashara kwa watoa huduma za mawasiliano nchini.

Baadhi ya miradi inayotekelezwa na UCSAF ni pamoja na ule wa kufikisha huduma za mawasiliano vijijini, mafunzo ya TEHAMA kwa walimu, kutoa vifaa vya TEHAMA na kuunganisha shule za umma na mtandao wa intaneti pamoja na kuboresha usikivu wa matangazo ya radio.

Imetolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote( UCSAF)
Previous articleMAASKOFU WA KANISA ANGLIKANA TANZANIA WATEMBELEA KABURI LA HAYATI MAGUFULI NA KUFANYA IBADA CHATO.
Next articleMAJALIWA: WAHARIRI ZINGATIENI VIWANGO NA UBORA KATIKA UANDISHI WA HABARI..

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here