Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesisitiza Jeshi la Magereza kuzingatia na kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Haki Jinai pamoja na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ili kuboresha huduma za urekebu na ufanisi wa Jeshi hilo.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza unaofanyika Makao Makuu ya Jeshi hilo, Msalato mkoani Dodoma. Amesema taarifa hizo zilianisha mambo mbalimbali yanayoplekea wafungwa wanaomaliza vifungo vyao kufungwa tena kuwa ni pamoja na kukosekana kwa miongozo rasmi ya magereza ya namna ya kutekeleza programu za urekebu, kutokuwepo na utaratibu mzuri wa kubaini na kuwatenga wafungwa kwa ajili ya programu za urekebu kulingana na vipaji vyao, kutokuwepo kwa programu za kutosha za huduma za kielimu na kisaikolojia kwa wafungwa pamoja na kukosekana kwa programu za kuwaandaa wafungwa wanaokaribia kumaliza vifungo. Amesema pia taarifa ya Tume ya Haki Jinai ilianisha utumiaji wa nguvu kupita kiasi ikiwa ni pamoja na ukaguzi unaotweza utu na kukiuka haki za binadamu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikagua Gwaride la heshima lililoandaliwa na Jeshi la Magereza mara baada ya kuwasili Makao Makuu ya Jeshi hilo, Msalato mkoani Dodoma kufungua Mkutano wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza. Tarehe 24 Oktoba 2024.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Magereza kuchukua hatua zinazowezekana kwa kutumia rasiliamli zilizopo, kuondoa dhana ya kudhalilisha utu na kukiuka haki za binadamu. Amesema ni muhimu kupunguza na hatimaye kuondokana kabisa na matumizi ya ndoo magerezani kama choo. Aidha amewasihi kushirikiana na wadau mbalimbali kufanya juhudi kuwapatia wafungwa vifaa vitakavyowasaidia kujiendeleza kielimu wanapokuwa magerezani kama kompyuta, vitabu na vifaa vingine.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewasihi Viongozi na Maafisa Magereza kubadili mtazamo ili kuendana na mazingira ya sasa. Amesema kinachohitajika zaidi ni dhamiri ya dhati na ubunifu ili kuwezesha upatikanaji wa huduma bora za urekebu na kupunguza idadi ya wanaomaliza vifungo vyao kurejea tena magerezani. Aidha ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhakikisha mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Magereza unakamilika mapema na unazingatia mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai na hali ya sasa.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na Viongozi na Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza wakati akifungua Mkutano wa Maafisa hao unaofanyika Makao Makuu ya Jeshi hilo, Msalato mkoani Dodoma. Tarehe 24 Oktoba 2024.
Vilevile amesisitiza umuhimu wa Jeshi la Magereza kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na Bodi ya Parole kuweka utaratibu wa kuwatambua na kuwafuatilia wale wanaotoka Magerezani kwa msamaha na hata wale waliomaliza vifungo vyao wanakokwenda na jinsi wanavyoenenda.
Pia Makamu wa Rais amesema ni muhimu Jeshi la Magereza kujitosheleza kwa chakula na kuimarisha usimamizi wa miradi inayoendeshwa na Jeshi hilo. Ameitaka Magereza iweke nguvu katika kuzalisha miche na mbegu hususan za mazao ya kimkakati ili kulisaidia Taifa kuondokana na utegemezi wa mbegu kutoka nje ya nchi. Amesema ni muhimu Jeshi la Magereza lijizatiti katika sekta ya ufugaji wa mifugo ya aina mbalimbali kwa ajili ya matumizi magerezani na kuuza ziada katika soko la ndani na nje ya nchi.
Makamu wa Rais ameliagiza Jeshi la Magereza kuongeza jitihada katika uhifadhi na utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi ya kupikia. Ameyataka Magereza yote kuwa kielelezo cha upandaji miti ya kivuli, matunda na maua katika maeneo yao pamoja na Magereza yaliyo kando ya barabara kuu kuhakikisha wanapanda miti pembezoni mwa hifadhi ya barabara. Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa kila gereza kutunza msitu wa asili ulio karibu au kuanzisha msitu wa kielelezo kwa kupanda miti, kwa kushirikiana na wananchi wa maeneo hayo na kuwataka uongozi wa wilaya na mkoa kusaidia kufanikisha kazi hiyo.
Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Katungu amesema Jeshi hilo limeendelea kuimarisha matumizi ya Mahakama mtandao katika magereza ambapo kufikia sasa jumla ya magereza 66 yana huduma hizo zinazosaidia wahalifu kuweza kusikiliza mashauri yao wakiwa magerezani.
Aidha amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 zimetengwa jumla ya shilingi bilioni 1.3 kwaajili ya kujenga vyumba vya mahakama mtandao katika magereza 20. Pia shilingi milioni 451.5 zimetengwa kwaajili ya kuweka mfumo wa taarifa za wahalifu.
Amesema katika jitihada za kuimarisha ulinzi na usalama magerezani, Jeshi hilo limefunga mfumo wa CCTV katika magereza 10 ambapo inatarajiwa kuendelea kuweka huduma hiyo katika magereza yote nchini.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereza mara baada ya kufungua Mkutano unaofanyika Makao Makuu ya Jeshi hilo, Msalato mkoani Dodoma. Tarehe 24 Oktoba 2024.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
24 Oktoba 2024
Dodoma.