Home INTERNATIONAL MHE.PHILIP MPANGO AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI WA NISHATI YA JOTOARDHI  KUSHIRIKIANA NA TANZANIA

MHE.PHILIP MPANGO AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI WA NISHATI YA JOTOARDHI  KUSHIRIKIANA NA TANZANIA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga wakati alipowasili katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam kufungua Kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika tarehe 23 Oktoba 2024. 

Dar es salaam.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewakaribisha wawekezaji kushirikiana na Tanzania katika kuwekeza kwenye nishati ya Jotoardhi inayopatikana katika maeneo mbalimbali nchini. 

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Ametaja baadhi ya maeneo muhimu ambayo yatazalisha nishati ya jotoardhi ni pamoja na Ngozi (Megawati 60), Kyejo – Mbaka (Megawati 60), Songwe (Megawati 5-35), Natron (Megawati 60) na Luhoi (Megawati 5).

Makamu wa Rais amesema Tanzania ipo tayari kwaajili ya uwekezaji katika sekta ya jotoardhi kutokana na kuwa na amani na utulivu, mazingira mazuri ya kuvutia, utulivu wa kisiasa pamoja na sera imara chini ya marekebisho ya kimuundo kupitia falsafa ya R nne za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambazo ni mageuzi, kujenga upya, maridhiano na ustahimilivu.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) Mhandisi. Shakiru Kajugus kuhusu mfano wa nishati ya jotoardhi inavyovunwa wakati wa Kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Tarehe 23 Oktoba 2024.

Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa rai kwa Nchi wanachama zenye rasilimali ya jotoardhi zinazopitiwa na bonde la ufa (ARGeo) kuwa na ushirikiano na juhudi zinazoratibiwa katika kuchunguza maeneo ya jotoardhi na kutafuta uwekezaji unaohitajika katika kutumia rasilimali hii muhimu. Amesema ni muhimu kuimarisha ubadilishanaji maarifa, mbinu bora, teknolojia pamoja na kubuni na kutekeleza programu za uchunguzi za kikanda.

Pia Makamu wa Rais amesema ni vema kwa kila nchi mwanachama kuwa na taasisi inayosimamia na kuongoza maendeleo ya jotoardhi ikiwa ni pamoja na mifumo sahihi ya kisheria na udhibiti ambayo inaweza kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) Mhandisi. Shakiru Kajugus kuhusu miradi inayotekelezwa na kampuni hiyo wakati akitembelea mabanda ya maonesho katika Kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Tarehe 23 Oktoba 2024.

Aidha amesema kutokana na bajeti za serikali kitaifa kutotosheleza kugharamia uwekezaji mkubwa unaohitajika katika awamu ya maendeleo ya miradi ya jotoardhi hivyo ni umuhimu kwa Nchi wanachama zenye rasilimali ya jotoardhi zinazopitiwa na bonde la ufa (ARGeo) kuwa na mazungumzo maalumu ya mara kwa mara na Benki za Maendeleo ya Kimataifa kama vile AfDB na Benki ya Maendeleo ya Miundombinu ya Asia hivyo kufanya uwekezaji binafsi katika matumizi ya rasilimali jotoardhi kuvutia zaidi.

Makamu wa Rais amesema Kwa sasa, Tanzania imekamilisha hatua za awali za utafiti wa rasilimali ya jotoardhi katika maeneo matano yaliyo kando ya bonde la ufa, na imeanza kuchimba visima katika moja ya maeneo yaliyopo Ziwa Ngozi upande wa Magharibi mwa ziwa hilo.

Pia uchunguzi unafanywa katika miradi ya kimkakati ambayo ni Kyejo-Mbaka, Luhoi na Natron. Ametaja mafanikio mengine ni kuongezeka kwa idadi ya Watanzania wenye utaalam wa jotoardhi na ununuzi wa mitambo ya kuchimba visima.
Kongamano hilo la siku saba lina kauli mbiu isemayo “Kuharakisha Maendeleo ya Rasilimali za Jotoardhi Afrika” linashirikisha jumla ya washiriki 800 kutoka mataifa 21 duniani.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na viongozi mbalimbali wakishiriki Kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Tarehe 23 Oktoba 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na viongozi mbalimbali wakishiriki Kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Tarehe 23 Oktoba 2024.

 

Previous articleDKT.MPANGO ATEMBELEA BANDA LA EWURA MKUTANO WA ARGeo-C10
Next articleBARABARA YA LAMI YA KM 7.7 YENYE THAMANI YA BILIONI 9.3 KUUNGANISHA MIKOA YA SINGIDA-SIMIYU-ARUSHA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here