Dkt. Mpango aagiza wasakwe awataka NMB kumsimamisha kazi Mtumishi wake aliyekula njama, asikitishwa mtendaji kuuwawa kikatili.
Watumishi wa umma na wengine 15 matatani, ataka taarifa zao zifike kwa Waziri Mkuu.
Na: Mwandishi wetu
Makamu wa Rais wa Dkt Philip Mpango, ameshtushwa na taarifa iliyotolewa na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ikihusisha watumishi wa umma na wengine 15 na Afisa Mikopo wa Benki ya NMB waliopiga fedha za tumbaku zaidi ya shilingi bilioni 1.2 mkoani Tabora.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara yake ya siku 4 mkoani humo Makamu wa Rais Dkt. Mpango amesema, ameshtushwa na taarifa iliyotolewa na Waziri Bashe na anaagiza hatua za uchunguzi kufanyika na vyombo vya dola viwasake waliohusika.
Amesema fedha hizo zilizopigwa ni mikopo ya wakulima wa Kisanga Amcos Sikonge mkoani Tabora.
“Asante Waziri Bashe kwa kulipua hili na hongera kwa kuchukua hatua kwako kwa kuwasimamisha kazi maafisa kilimo na ushirika, namuagiza Mtenda Mkuu wa NMB huyu Afisa Mikopo Tabora aliyekula njama za wizi huu asimamishwe kazi mara moja na watumishi wa umma wote waliopiga fedha hizo na wengine kuhamishwa wasakwe na kushikiliwa kwa uchunguzi,” amesema.
Amesema, pia taarifa kamili ya sakata hilo ifikishwe mikononi mwa Waziri Mkuu Khassim Majaliwa.
Dkt.Mpango amesema ni jambo la aibu na ukosefu wa maadili kuona walioshiriki wizi huo ni watumishi wa umma tena wanawaibia wanyonge ambao ni wakulima.
“Naungana na Waziri wa Kilimo Bashe mali za wahusika wote zishikiliwe na vyombo vyetu vifanye kazi yake wakulima walipwe fedha zao,pia nimeumia zaidi kusikia hapa yupo Mtendaji ameuwawa kikatili, sijui ni uhalifu wa aina gani.
“Naomba niwasilishe pole yangu ya sh. Milioni 5 kwa mke na familia ya aliyeuwawa,”amesema.
Hatua hiyo, imefikiwa baada ya Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, kuwalipua waliohusika katika ubadhilifu wa fedha za tumbaku sh. Bilioni 1.2 na kusisitiza kuwa wizi huo umefanywa bila woga na watumishi walioshiriki wapo kazini.
Waziri Bashe amesema watuhumiwa hao walikuwa wajanja, kwani hakuna uingizaji wa fedha wa moja kwa moja uliofanywa unaoweza kuonekana kutoka kwenye akaunt ya chama kwenda kwenye akaunt zao, lakini akaunti zao zilikutwa na fedha nyingi na miamala ilibainika kuingia kama cash bila chanzo kujulikana.
“Baada ya vyombo vya usalama na TAKUKURU kuwabana viongozi wachama walikiri kuwa walikuwa wanashiriki biashara hiyo na watumishi wetu kwa usaidizi wa Afisa Mikopo wa NMB.
“Na wote walikuwa wanajishughulisha na biashara kwenye vyama vya msingi kama kuuza magunia yakufungia tumbaku na mahindi ya chakula, kimajukumu Afisa ushirika alikuwa ni mkaguzi , mlezi wa vyama na pia mpitishaji wa malipo na ukomo lakini aliamua kujinufaisha mwenyewe na afisa mikopo katumia fursa hiyo huku chama kikiangamia wakulima ndio waathirika,”amesema.
“Kati ya 15 waliohusika wapo watumishi ambao baadhi wamehamishwa kikazi mmoja akiwa Mbeya na mwingine ametolewa Sikonge na kupelekwa Igunga.
“Pia wapo waliokuwa viongozi wa Chama cha Msingi Kisanga huyu wa Mbeya kwa kuwa ni Mrajisi aliyekuwa Afisa ushirika wa wilaya nina mamlaka naye nimesema arudishwe na apishe uchunguzi,”amesisitiza.
Ameongeza kuwa “ Fedha hizo ni mikopo ya wakulima na wahusika wamechukua fedha nyingi na kuingizia wakulima hewa ambao baadhi ni makalani na ndugu zao.
“Ni kama wamepitisha huko na baadaye kuingizwa katika akaunti zao kwa cash waliobaini ni wakulima wenyewe na waligoma kulipa mkopo huo na kutorosha tumbaku zao,wale wasiojua kitu walipeleka sokoni lakini kila wakiuza zinazuiliwa na hazilipwi, wakilipa deni sasa wakulima hawawezi kuwa wahanga wa huu mkopo ninachojua fedha zao zitalipwa.
“Wezi watafutwe, nimeagiza wakulima wasikose pesa za kupandia, kulimia na mbolea za kukuzia tusiumize wasiohusika ikiwa wahusika wapo,”amesema.