Home LOCAL TCRA YAZINDUA KAMPENI YA “NI RAHISI SANA” KANDA YA KASKAZINI KUHIMIZA KUJILINDA...

TCRA YAZINDUA KAMPENI YA “NI RAHISI SANA” KANDA YA KASKAZINI KUHIMIZA KUJILINDA NA UHALIFU MTANDAONI

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Kaskazini Mhandisi Francis Mihayo akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Ni Rahisi Sana
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Kaskazini Mhandisi Francis Mihayo akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Ni Rahisi Sana
Na Mwandishi wetu-malunde 1 blog

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Kaskazini imezindua Kampeni Kabambe ilijulikanayo kama ‘Ni Rahisi Sana’ yenye lengo la kuwahimiza watanzania wote wajilinde dhidi ya uhalifu mtandaoni.

Akizungumza wakati wa Uzinduzi huo wa Kampeni ‘NI RAHISI SANA’ leo Jumatano Oktoba 9,2024 katika jengo la PAPU Jijini Arusha, Meneja wa TCRA Kanda ya Kaskazini inayojumuisha mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga) Mhandisi Francis Mihayo amesema moja ya majukumu ya TCRA ni kujenga jamii inayowezeshwa vyema na huduma za mawasiliano kupitia udhibiti kwa ajili ya ustawi wa jamii ya Tanzania.

“Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaungana na Dunia katika kuadhimisha Mwezi wa Elimu ya Usalama Matandaoni, ambayo huadhimishwa Oktoba kila mwaka kwa kuwahimiza wananchi wajilinde dhidi ya uhalifu mtandaoni. Kama mdhibiti wa huduma za mawasiliano nchini Tanzania na muwezeshaji uchumi wa kidijitali, TCRA katika kutekeleza majukumu yake hivi karibuni Mkurugenzi mkuu  wa TCRA Dk Jabiri Bakari alizindua kampeni kabambe ijulikanayo “ Ni Rahisi Sana” na leo hii tumezindua Kampeni hii katika Kanda ya Kaskazini”,amesema Mhandisi Mihayo.

“Kampeni hii ya Ni Rahisi Sana imelenga kuwahimiza watanzani wote tujilinde dhidi ya uhalifu mtandaoni kwani uwepo wa mazingira salaama mtandaoni yatawezesha kufikia malengo ya uchumi wa Kidijiti.Katika wakati tuliopo sasa wa kidigitali matumizi ya teknolojia yamekua yakiongezeka kwa kasi na ni muhimu sana katika maisha yetu ya kila siku”,amesema Mhandisi Mihayo. 

Amebainisha kuwa Kampeni ya Ni Rahisi Sana itakapotekelezwa kwa mujibu wa mpango uliopendekezwa itakuwa na matokeo mengi ikiwemo Kuongeza uelewa kwa umma juu ya kutosambaza taarifa za uongo, Uelewa wa umma juu ya kugundua maudhui ya upotoshaji, Kujua utaratibu wa kuripoti kwa watumiaji wanapokumbana na taarifa za uongo wanapotumia huduma za mawasiliano, Uelewa Zaidi kwenye jina la kikoa cha DOT TZ, ili kupunguza Ufutaji wa kikoa cha DOT TZ, Kuongeza idadi ya usajili wa kikoa cha DOT TZ na Kuongeza idadi ya watumiaji na mwingiliano kupitia mitandao yetu ya kijamii.

Amefafanua kuwa, Kampeni ya ‘Ni Rahisi Sana’ imegawanyika katika awamu mbili kwa muda wa miezi sita (1 Oktoba, 2024 mpaka 30 Machi, 2025) ambapo Kipindi cha kwanza kitakuwa kuanzia (1 Oktoba 2024 hadi 31 Disemba 2024) na kipindi cha pili kitakuwa kuanzia (1 Januari 2025 hadi 30 Machi 2024)

Mhandisi Mihayo ameeleza kuwa, Kampeni hii Ni Rahisi Sana inalenga kuwapa watu Maarifa muhimu ya kuzunguka katika majukwaa mbalimbali ya  kidijitali yanayohusu  usalama mtandaoni; Kuongeza usajili wa jina la kikoa cha DOT TZ, kuongeza uelewa juu ya jinsi TCRA inavyosaidia bunifu mbali mbali zinazohusu TEHAMA, Kuongeza uelewa juu ya kuripoti vitendo vya ulaghai na kukomesha kueneza habari za uongo kwa jamii na Kuthamini wateja na wadau wengine nchini Tanzania.

Amesema Kampeni ya Ni Rahisi Sana italenga zaidi watoto, vijana na wazee wakiwemo watu wenye mahitaji maalum ambapo pia itazingatia Mashirika au Mashirika ya Biashara, Mashirika yasiyo ya Faida (NGOs), Wanafunzi, Wamiliki wa Biashara, Watoa maamuzi, Waliopewa Leseni na TCRA na Mashirika ya Kitaalamu.

Kwa kuelewa matumizi ya jamii ya Watanzania, TCRA imeandaa ujumbe mahususi kwa kila eneo la kuongeza elimu na utatolewa kupitia vyombo vya habari, ujumbe kwenye simu za mkononi na kwenye maeneo ya umma kama stendi za mabasi, minada mbali mbali nk.

 Kauli mbiu ya kampeni “Ni Rahisi sana” itakuwa inasisitiza mambo mbalimbali mfano;

Ni rahisi sana kumtambua tapeli kwani atakupigia namba ya kawaida badala ya namba 100;

Ni rahisi sana kutoa taarifa kwa mtu anayetaka kukutapeli tuma namba yake kwenye namba 15040;

Ni rahisi sana kuwasiliana na TCRA endapo una malalamiko yanayomuhusu mtoa huduma wako au ukitaka kupata elimu au ushauri wa kutaka kuanzisha biashara ya mawasiliano piga namba ya bure 0800008272;

Ni rahisi sana kujua maudhui mtandaoni yanayolenga kupotosha 

Ni rahisi sana kujua habari feki;

Ni rahisi sana kwa shule za awali, msinigi, sekondari na vyuo kuanzisha club za Kidijitali;

Ni rahisi sana kujisajili na kuanza kutumia Kikoa cha DOT TZ;

Ni rahisi sana kwa wabunifu wote katika nyanja za TEHAMA kupata kupata rasilimali kama namba na masafa kwaajili ya kufanyia majiribio bunifu zao;

Ni rahisi sana kuhuisha mifumo ya kifaa cha mawasiliano

Ni rahisi sana kusoma vigezo na masharti 

Ni rahisi sana kuchukua tahadhari kwa watoto wetu wanapotumia mitandao

Ni rahisi sana kujilinda dhidi ya majaribio ya udukuzi 

Ni rahisi sana kutambua usahihi wa taarifa

Ni rahisi sana kutambua vyanzo vya habari 

Ni rahisi sana kujielimisha na kusoma zaidi 

Ni rahisi sana kutumia teknolojia kuhakiki taarifa mtandaoni “,amesema Mhandisi Mihayo.

Mhandisi Mihayo ameeleza kuwa, watu wengi nchini Tanzania hawana ujuzi wakutosha wa matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii pamoja na namna ya kulinda  usalama wao mitandaoni, jambo linalowafanya kuwa hatarini kwa mashambulizi, ulaghai wa mtandaoni na pia matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii. 

 “TCRA kupitia kitengo cha Mawasilino na Mahusiano ya Umma (CPRU) inatambua umuhimu wa kukuza elimu ya kidijitali na usalama mitandaoni ili kuhakikisha mazingira ya kidijitali yana usalama na kuhamasisha juu ya fursa zilizopo kwa matumizi sahihi mtandao kwa wananchi wote kushiriki kwa usalama kiuchumi na kisiasa hasa katika kipindi cha chaguzi mbalimbali”,amesema Mhandisi Mihayo.

“Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imekuwa ikitoa elimu katika maeneo mengi kwa uwazi kwa miaka mingi, ingawa utoaji wa elimu umeendelea kuwa endelevu wakati wote. Mabadiliko ya kasi ya teknolojia yamekuwa yakienda sambamba na ongezeko la vitendo vya ulaghai mitandaoni, ambapo wahusika wamekuwa wakibuni mbinu mpya kila wakati na kusababisha elimu ya usalama iwe endelevu wakati wote kwa jamii nzima. Mamlaka itaendelea kuelimisha umma kwa kusisitiza matumizi chanya ya teknolojia”,ameongeza Mhandisi Mihayo.  

 

 

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here