Na. OR TAMISEMI, Tabora
Mkurugenzi Msaidizi, Elimu ya Watu Wazima, Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mwalimu Ernest Hinju amewataka Maafisa Elimu Watu Wazima wa Mikoa na Halmashauri nchini kufanya kazi kwa ufanisi na weledi ili kuleta mageuzi kwenye Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi.
Mwalimu Ernest Hinju ametoa wito huo leo tarehe 08, Oktoba 2024 wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili cha Maafisa Elimu Watu Wazima chenye lengo la kutathmini utendaji kazi wao, kilichofanyika Manispaa ya Tabora katika ukumbi wa Isike Mwanakiyungi uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
Mwalimu Ernest Hinju amewataka Watendaji hao kutumia fursa ya kikao kazi hicho kufanya tathmini ya utendaji kazi wao nchini ili kuleta mapinduzi makubwa kwenye Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi.
“Kikao hiki kitumike kufanya tathmini ili kuona kwa kiasi gani tunatekeleza kwa ufanisi shughuli zote za Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi na hatimaye mje na mikakati ya kuboresha utendaji kazi,” Mwalimu Ernest Hinju amesisitiza.
Mwalimu Hinju amesema kikao hicho pia kinapitia maazimio ya kikao kama hicho kilichofanyika mkoani Morogoro mwaka 2024 kikitoa fursa ya kupeana ujuzi, uzoefu, kutambua nafasi zao, kujua changamoto za Elimu ya Watu wazima pamoja na kudumisha umoja, ushirikiano na upendo miongoni mwa Maafisa hao ili kuboresha utendaji wao kwa manufaa ya watanzania. Aidha, kikao hicho kilitoka na maazimio ambayo pia utekelezaji wake utawasilishwa katika kikao kazi hiki.
Akiongea kwa niaba ya Afisa Elimu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aron Vedasto amezishukuru Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuandaa kikao kazi hicho kama sehemu ya maadhimisho ya juma la Elimu ya Watu Wazima mkoani Tabora kwani wataweza kujitathmini kama mkoa. lakini ameahidi kuhakikisha wanainua Elimu ya Watu Wazima.
Sanjari na hilo, Bw. Aron Vedasto ameahidi kuwa, watahakikisha wanainua Elimu ya Watu Wazima kwani kwa mujibu wa takwimu za sensa mwaka 2022 zinaonyesha mkoa huo ndio unaoongoza kuwa na idadi kubwa ya watu wasiojua Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa miongo miwili mfululizo.
Naye Bw. Florence Njiku Afisa Elimu Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi Mkoa wa Mara, akiwasilisha taarifa ya mkoa amesema mkoa wake una jumla ya wanakisomo wa MUKEJA 1357, MEMKWA 2463, wasichana waliokatishwa masomo kupitia SEQUIP 179 huku walimu na watu mbalimbali wakitumia Programu ya Elimu Masafa na Elimu ya ana kwa ana (ODL), hivyo wamefanikiwa kuwa na jamii yenye mwamko wa kuwarejesha masomoni wanafunzi wengi walioacha shule na wale waliokatishwa masomo.
Kikao kazi hicho cha siku mbili ni sehemu ya maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima Kitaifa yanayofanyika mkoani Tabora ambayo yameandaliwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikihusisha baadhi ya Taasisi za Wizara hizo na Wadau mbalimbali huku kukiwa na kongamano na maonyesho.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Ujumuishi katika Elimu bila ukomo kwa ujuzi, ustahimilivu, amani na maendeleo”