Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB, Godfrey Ndalahwa, akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wanahisa wa benki hiyo wakati wa uzinduzi wa muonekano mpya wa benki hiyo uliofanyika pamoja na Mkutano Mkuu wa 19 wa Wanahisa wa DCB jijini Dar es Salaam leo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB, Godfrey Ndalahwa (wa nne kushoto), Mwenyekiti wa Bodi ya DCB, Maharage Chande (kushoto kwake), pamoja na wakurugenzi wa benki hiyo, wakishangilia wakati wa uzinduzi rasmi wa muonekano mpya wa benki hiyo uliofanyika pamoja na Mkutano Mkuu wa 19 wa Wanahisa wa DCB jijini Dar es Salaam leo.
Baadhi ya wakurugenzi wa DCB pamoja na waalikwa wengine wakisikiliza hotuba ya Mkurugenzi Mtandaji wa benki hiyo, Godfrey Ndalahwa wakati wa uzinduzi rasmi wa muonekano mpya wa benki hiyo uliofanyika pamoja na Mkutano Mkuu wa 19 wa Wanahisa wa DCB jijini Dar es Salaam leo.
Mmoja wa wanahisa wa Benki ya DCB na Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye (wa pili Julia), akizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya benki hiyo, Maharage Chande (wa pili kushoto) wakati wa Mkutano Mkuu wa 19 wa Mwaka wa Wanahisa wa Benki hiyo uliofanyika pamoja na uzinduzi wa Muonekano Mpya wa Benki ya Biashara ya DCB, kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam leo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Biashara ya DCB, Maharage Chande (katikati) akizungumza na wanahisa wa benki hiyo wakati wa Mkutano Mkuu wa 19 wa Benki ya DCB uliofanyika pamoja na uzinduzi rasmi wa NEMBO mpya ya benki hiyo, jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Godfrey Ndalahwa na kulia ni mjumbe wa bodi, Zawadia Nanyaro.
Na Mwandishi Wetu | Benki ya Biashara ya DCB leo imezindua muonekano wake mpya , ambao unaenda sambamba na mikakati ya benki hiyo ya kuboresha huduma zake na kukidhi malengo na maono iliyojiwekea mara baada ya kupewa leseni ya kujiendesha kama benki kamili ya biashara.
“Muonekano huu mpya unawiana na mabadiliko na mafanikio yatokeayo kwenye benki hii yanayolenga kuisimika DCB kwenye njia ya ukuwaji na utowaji wa huduma bora zinazorandana na mabadiliko ya soko la kibenki,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa DCB, Godfrey Ndalahwa, kwenye uzinduzi leo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika pamoja na Mkutano Mkuu wa 19 wa Mwaka wa Wanahisa wa benki hiyo Ndalahwa alisema, muonekano huo mpya ni sehemu ya utekelezaji wa mpango kazi wa DCB wa miaka mitano 2018-2022, unaolenga kuikuza na kuibadilisha benki ili kwenda sawia na hali ya soko.
Akifafanua, Ndalahwa alisema muonekano huo mpya utalenga kuwezesha benki hiyo kuwafikia Watanzania wengi zaidi nchi nzima, kutoa huduma bora zaidi za kiubunifu na zenye gharama nafuu katika mrengo wa kidigitali, kuendelea kuongeza thamani ya uwekezaji ili kukuza mapato ya wanahisa, kuimarisha benki, na kuhakikisha fedha za wateja zipo salama.
Mkurugenzi huyo alieleza kuwa nembo mpya ya DCB ina mistari sambamba miwili inayoakisi dhana ya kuwa DCB ni benki ya biashara inayoongozwa kwa misingi imara na uzoefu na uthibitisho wa mafanikio makubwa toka kuanzishwa kwake, na ina doti jekundu kuashiria safari ya benki hiyo katika kuwa mstari wa mbele kutoa huduma za kidigitali na kuwafikia wateja wengi zaidi.
“Vilevile, benki pia imebadili rangi kwenda nyekundu na bluu ikiwakilisha uwezo na nguvu ya kutoa huduma, uzoefu katika soko, utulivu tunapohudumia wateja wetu, uimara wa misingi tuliojiwekea, uaminifu kwa wateja wetu na shauku ya kutoa huduma bora kwa wateja wetu,” alisema Ndalahwa.
“Muonekano huo mpya wa DCB utaonekana kwenye vituo vyetu vyote vya kutolea huduma, matawi, ATM, mawakala, huduma za mtandao wa simu (DCB Digital), mitandao ya kijamii, tovuti na sehemu nyingine zote.“
Benki ya Biashara ya DCB ilianzishwa mwaka 2002 kuitikia kilio cha wakazi wengi wa Jiji la Dar es Salaam cha kukosa chanzo cha mitaji midogo ya biashara, hali iliyokuwa changamoto kubwa kwa wajasiriamali wadogo katika jitihada za kuboresha maisha yao, hasa kwa kuzingatia masharti magumu ambayo yalikuwa yanawekwa na benki nyingi za kibiashara.
“Kwa kipindi chote cha miaka 19 ya uendeshaji, jukumu mama la benki hii limeendelea kuwa ni kutoa huduma bora za kifedha huku ikijikita zaidi katika kutengeneza miradi endelevu ya kupunguza umaskini na kuendeleza jamii.Benki imeendelea kushindana kwenye soko kwa kuhakikisha inatoa huduma bora na bidhaa zenye ubunifu kwa wateja wake,” a lisema Ndalahwa.
Alitaja mafanikio makubwa kuwa ni, kuboresha leseni na kupanda hadhi kutoka benki ya mkoa hadi kuwa benki kamili ya biashara, kuwa benki ya kwanza kujiunga na Soko la Hisa la Dar es salaam, kulipa gawio mfululizo tangia kuanzishwa kwake, kutoa huduma na bidhaa zinazokidhi viwango vya ushindani, na kufungua matawi 8 na vituo vya kutolea huduma 12.
Pamoja na hayo, alisema DCB imekuwa ikitoa huduma bora kwa wateja mbalimbali wadogo, wa kati na wakubwa, ambao hadi sasa benki ina wateja zaidi ya 200,000; imeweza kufikia mizania inayokaribia billioni 200; ina huduma za simu ya mkononi (DCB DIGITAL); ina huduma za internet banking na Visa, na ATM zinazounganishwa kwenye huduma za Umoja Switch zinazopatikana kwenye ATM 300 nchi nzima.
Ndalahwa alibainisha azma ya dhati ya Benki ya Biashara ya DCB ya kuendelea kubuni huduma bora kwa lengo la kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za benki hiyo nchini kote.
“Tumeimarisha huduma zetu, na sasa mteja anaweza kupata huduma za kibenki popote alipo kupitia DCB Digital, huduma za kibenki kwa njia ya intaneti na simu za mkononi, mawakala nchi nzima na matawi yetu ili kuondoa usumbufu wa wateja wetu kuja matawini. Tunawaahidi kuendelea kuwa wabunifu na kuendelea kukidhi mahitaji ya wateja wetu kulingana na matakwa na matarajio yao,” alisema.