Akizungumza kwa njia ya simu wakati wa hafla ya ugawaji wa mitungi na majiko hayo yaliyotolewa na Mbunge wa Arusha Mjini kwa uratibu wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania , Rais Samia amesema amepongeza hatua hiyo ya walimu wa Arusha kupatiwa majiko ya gesi na kuahidi kuongeza majiko zaidi kwa walimu hao kwa siku za baadae.
“Nimepiga simu niwapongeze walimu kwa Mkutano mzuri ,Mbunge ameniambia leo mnamkutano wa nishati safi ya kupikia kwa hiyo niwapongeze kwa kuibeba hiyo ajenda.Niwaahidi tu mchango wangu katika hilo ndugu walimu katika majiko yatakayotoka mimi nitakuja kujazia baadae,”amesema Rais Samia huku akiwaeleza pia walimu kuwa ajenda zao na changamoto zao anazifahamu na wanaendelea kuzifanyia kazi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Omar Kipanga aliyekuwa mgeni katika maadhimisho ya walimu jijini Arusha kwa niaba ya Waziri wa Elimu Profesa Adolf Mkenda amesema wanamshukuru Rais Samia kwa jitihada anazofanya za kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
“Katika siku hii ya leo ya kuadhimisha siku ya walimu kauli mbiu yetu inahusu masuala ya nishati safi ya kupikia na kama mnavyofahamu Rais DK.samia Suluhu Hassan amezungumza na sisi leo lakini tunakumbuka Mei mwaka huu alizindua Kampeni hii ya utumiaji wa nishati safi ya kupikia na malengo yetu kama Serikali ni kuhakikisha itakapofika mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wamefikiwa katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.
“Hivyo tunamshukuru pia Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo pamoja na Oryx kwa kutoa mitungi ya gesi kwa walimu 5000 ili watumie nishati safi ya kupikia.Kama nilivyosema kampeni Kya Rais aliyotangaza Mei 8,2024 ni kwamba kila Mtanzania atumie nishati safi ya kupikia …
“Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia tumelibeba jambo hili na tumeanza na taasis zote za elimu ambazo zinahudumiwa watu zaidi ya 100 kuanza kutumia nishati safi ya kupikia.Walimu 5000 wa Arusha ambao wamepatiwa majiko ya gesi wanaandaliwa utaratibu wa kupatia elimu ya matumizi sahihi ya nishati ili waweze kuishusha kwa wananchi na wote tutumie nishati safi ya kupikia.
“ Dk.Samia Suluhu Hassan alishatoa elimu ya nishati safi ya kupikia kwa Wabunge wote na katika Bunge lililopita kila Mbunge alipewa majiko 200 kwa ajili ya kwenda kugawa katika majimbo yao na lengo kubwa ilikuwa kuhamasisha wanasiasa lakini kama mnavyofahamu jambo lolote haliwezi kwenda kama hakutakuwa na utashi wa kisiasa,hivyo Rais anatuongoza katika Kampeni hii,”amesema Kipanga.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman amesema kwa kushirikiana na Mbunge wa Arusha Mjini wameweza kıratibu walimu 5000 kupatiwa majiko hayo yenye thamani ya Sh.milioni 417.5 lakini dhamira yao ni kuona makundi mbalimbali yakiwemo ya walimu wanatumia nishati safi ya kupikia.
“Naomba niwagusie Waalimu na Maprofesa sio tu kwa sababu tunawasherehekea leo siku ya Walimu bali naamini ninyi nyote ni kiungo muhimu kwa jamii na Taifa letu.Hivyo natoa ombi maalum kwa walimu kuwa mabalozi wa Nishati Safi ya kupikia.”
Akitaja baadhi ya faida ya kutumia nishati safi ya kupikia amesema nishati safi husaidia kuboresha afya kwani nchini Tanzania wananchi 33000 wanafariki kila mwaka kutokana na kuvuta moshi na chembechembe zinazotokana na kuni na mkaa.Hivyo kupika kwa gesi ya kupikia oryx itaondoa changamoto hiyo.
Pia amesema kupika kwa nishati safi husaidia kutunza mazingira lakini wanafunzi watapata nafasi ya kutosha katika masomo badala ya kutumia muda mwingi katika kutafuta kuni porini.
Kwa upande wake Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo amesema wanatambua mchango walimu wote na katika kusherehekea siku ya walimu wameona kuna kıla sababu ya kuwapa zawadi ya jiko la gesi kwa kila mwalimu na wao wakawe mabalozi wa nishati safi.
“Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amezindua mpango wa nishati ya kupikia na bado mpango huo ukaweka malengo mpaka kutoka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
“Kazi ya Rais ni kuonesha njia na sisi wasaidizi wake ni kumuunga mkono na leo tunakabidhi majiko ya gesi kwa walimu na hii ni kumuonesha mwalimu tunampenda na tunamtambua na sasa wakawe mabalozi wa nishati safi ya kupikia.Tunawashukuru Oryx kwa kumuunga mkono Rais Samia kwani gharama za majiko haya 5000 ni Sh.milioni 417.5 ,”