Home LOCAL MAAFISA UGANI WOTE LAZIMA WAWE NA MASHAMBA DARASA-MAJALIWA

MAAFISA UGANI WOTE LAZIMA WAWE NA MASHAMBA DARASA-MAJALIWA

 

 SINGIDA.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI wahakikishe Maafisa Ugani wote nchini wanakuwa na mashamba darasa kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wakulima katika maeneo yao.

“Maafisa Ugani lazima wawe mashamba kwa ajili ya kufundishia wakulima na Afisa Ugani anayeshindwa kuonesha shamba huyo hafai kuwa Afisa Ugani”

Ametoa agizo hilo jana (Jumapili, Juni 13, 2021) wakati akizungumza na wadau wa zao la alizeti katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Kituo cha Mafunzo ya Kanisa Katoliki, Mkoani Singida.

Waziri Mkuu alisema wananchi waliacha kulima kwa sababu elimu ilikuwa haiwafikii, hivyo amewaagiza Wakuu wa Wilaya katika maeneo yote yanayolima alizeti wasimamie uundwaji wa vikundi vya wakulima wa zao hilo. “Vikundi ndio njia rahisi ya kuwafikia wakulima iwe kwa kuwapa elimu au mikopo.”

“Hakikisheni mnakuwa na kanzi data za wakulima katika maeneo yenu. Kanzi data hiyo itawawezesha kujua idadi ya wakulima, ukubwa wa mashamba yao pamoja na mahitaji yao. Pia jengeni utaratibu wa kuwatembelea wakulima ili kujua changamoto zinazowakabili na kushirikiana nao katika kuzitafutia ufumbuzi.”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwaagiza viongozi wa mikoa yote nchini waandae mpango mkakati wa kuendeleza mazao ya mafuta na kuuwasilisha Wizara ya Kilimo kwa ajili ya uratibu, usimamizi na ufuatiliaji. “Na kila kiongozi anapofanya ziara katika wilaya asomewe taarifa kuhusu hatua waliyofikia.”

“Halmashauri za Wilaya zitenge maeneo ya kuzalisha mbegu bora na kuanzisha mashamba makubwa ya pamoja (Block farms) ili kuongeza uzalishaji na kurahisisha utoaji wa huduma za ugani, mitaji na upatikanaji wa malighafi kwa viwanda vya mafuta ya kula.”

Kadhalika, Waziri Mkuu alizielekeza taasisi za utafiti wa masuala ya kilimo ziendelee kufanya tafiti za udongo ili kubaini ni aina gani ya mbegu zinazofaa kupandwa kwenye eneo husika. Amesema tafiti zinawawezesha wakulima kupanda mbegu sahihi katika mashamba yao, hivyo kupata mavuno mengi na bora.

Naye, Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema wizara imejipanga katika kuongeza uzalishaji wa mbegu bora kutoka tani 344 za sasa hadi kufikia wastani wa tani 2,000 hadi 2,500 kwa mwaka, hivyo ndani ya miaka mitatu ijayo nchi itakuwa imejitosheleza kwa mahitaji ya mbegu za bora alizeti.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Binilith Mahenge aliiomba Serikali kuunda bodi itakayosimamia mazao ya mafuta ili kuboresha usimamizi wa mazao hayo.  Pia aliishauri Serikali kupitia taasisi zake kama Jeshi la Magereza zianzishe mashamba ya mbegu za alizeti ili kurahisisha upatikanaji wake.

Previous articleWAAJIRI SEKTA BINAFSI SASA KULIPA ASILIMIA 0.6 YA MICHANGO YA WAFANYAKAZI KWENYE MFUKO WA WCF; SERIKALI
Next articleUTEKELEZAJI BAJETI YA WIZARA YA KILIMO; WAZIRI MKENDA AKUTANA NA BALOZI WA QATAR PAMOJA NA KAIMU BALOZI WA SAUDI ARABIA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here