NA: EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Tanzania inahitaji wawekezaji katika eneo la uzalishaji wa mbolea ili tuweze kujitoshereza kwenye eneo hilo kwani mpaka sasa zaidi ya asilimia 90% tunapokea mbolea kutoka nje ya nchi kwani tumekuwa na kiwanda cha mbolea kimoja ambacho kinazalisha chini ya asilimia 10 ya mahitaji.
Ameyasema hayo leo Juni 29,2022 Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt.Ashatu Kijaji mara baada ya kufanya mazungumzo na ugeni kutoka nchini Ghana wakiongozwa na Naibu Waziri wa Nishati na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara ambapo wamekuja kwaajili ya uwekezaji na Biashara kati ya Tanzania na Ghana.
Ugeni huo umeambatana na Wawekezaji na Wanyabiashara wakubwa kutoka nchini Ghana ambao wanazalisha bidhaa kwenye maeneo ya Nishati pamoja na Kilimo hasa kwenye mbolea.
Waziri Kijaji amesema wamejadili kuhusu uwekezaji katika eneo la viwanda vya mbolea pamoja na eneo la Nishati ambapo kwa pamoja ni maeneo makubwa ambayo wanafanya nayo kazi.
Aidha amesema kuwa kukiwa na wawekezaji wa kutosha ndani ya taifa kutaweza kuhudumia Afrika kutoka Tanzania lakini pia Tanzania tunasema ni lango la kuingilia na kutoka Afrika kwahiyo tunaweza kuihudumia Dunia kutoka Tanzania.
“Wawekezaji kama hawa sisi tunawapokea kwa mikono miwili kuhakikisha wanaanza uwekezaji na ninaamini hawana muda mrefu wanakuja kuwekeza ndani ya nchi yetu ili tuweze kujitoshereza kwa mbolea na kuwahudumia wenzetu waafrika kutoka Tanzania”. Amesema