Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ikiongozwa na Mwenyekiti, Mhe. Timotheo Mnzava (Mb) imeridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyo chini ya Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) inayotekelezwa ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha huku ikiitaka Wizara ya Maliasili na Utalii na Menejimenti ya Ruaha kuwa wabunifu kufanya maboresho yatakayoiongezea mapato Hifadhi ya Taifa Ruaha.
Ameyasema hayo leo Septemba 8, 2024 wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ya kukagua miradi ya ujenzi wa kituo cha ikolojia- Ibuguziwa, kituo cha utoaji taarifa kwa wageni,uwanja wa ndege wa Kiganga, ujenzi wa malazi ya watalii (cottage), malazi ya madereva na hosteli za wanafunzi za hifadhi hiyo Mkoani Iringa.
“Kutokana na ukubwa na umuhimu wa hifadhi hii, tuongeze ubunifu na maarifa ili kurahisisha watalii kufika kwa kuboresha miundombinu ya barabara na kuongeza njia za kuingilia hifadhini” amesema Mhe. Mnzava.
Aidha, ameweka msisito katika usimamizi wa miradi hiyo kuhakikisha inakamilika kwa wakati.
Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) ameishukuru kamati hiyo kwa maoni ya kuboresha hifadhi hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi.
Mhe. Chana ameendelea kutoa rai kwa wakandarasi wote waliokabidhiwa miradi iliyo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kukamilisha miradi hiyo kwa wakati kama ilivyo katika mikataba yao.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii inaendelea na ziara ya kukagua miradi mbalimbali iliyo chini ya Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW).