Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amesema Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano kati na India katika maeneo ambao yataongeza tija katika uchumi wa nchi kama vile kuanzisha viwanda vidogo vidogo vitakavyosaidia kuongeza thamani mazao yanayozalishwa nchini kabla ya kuuzwa nchini India.
Waziri Mkumbo ameyasema hayo alipokuwa akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, katika Mkutano wa Biashara na Uwekezaji kati ya India na nchi za Afrika (CII – Exim Bank Digital Conclave) uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 13 – 15 Julai 2021.
Akichangia katika Mkutano huo, uliolenga kujadili jinsi India na Nchi za Afrika itakavyoweza kukuza ushirikiano katika kukuza uchumi kwa kuzingatia maeneo ambayo kila nchi ina vivutio zaidi vya kiuchumi (Comperative advantage), Waziri Mkumbo, alisema Tanzania inatambua ushirikiano kati ya Tanzania na India na imeendelea kunufaika na ushirikiano huo hasa katika upatikanaji wa mikopo ya bei nafuu katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akitaja baadhi ya miradi inayotekelezwa kutokana na ushirikiano huo, Prof Mkumbo aliainisha Ujenzi wa mradi mkubwa wa kutoa maji katika ziwa Victoria kwenda mkoani Tabora unaotarajiwa kunufaisha zaidi ya wakazi milioni moja(1) wa wilaya za Nzega, Igunga, Uyui na Tabora mjini ambao unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 600. Aidha Tanzania imeendelea kunufaika na masoko ya mazao ya aina mbalimbali kama vile Korosho na mazao ya jamii ya Kunde. Alisema Prof. Mkumbo.
Pro. Mkumbo aliungana na Mawaziri kutoka nchi nyingine za Afrika kuelezea utayali wa Tanzania kushiriki kimataifa katika Makubaliano ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) ambao mchakato wake umefika katika hatua nzuri. Pia alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji wa India kuja kuanzisha shughuli zao nchini ili wanufaike na soko hilo.
Mkutano huo ulihudhuliwa na viongozi mbalimbali wa India na Afrika wakiwemo Makamu wa Rais wa nchi za Zimbabwe na Botswana na Mawaziri wenye dhamana za Viwanda, Biashara, Uwekezaji, Fedha, Nishati, Madini, Kilimo na Miundombinu kutoka nchi za Angola, Botswana, Burkina Faso, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Congo, Ivory Coast, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Guinea ya Ikweta, Eswatini, Ethiopia, Ghana, Kenya, Malawi, Mauntius, Morocco, Nigeria, Senega, Togo na Zimambwe.