Awataka viongozi na watendaji wa Mkoa huo kutumia mafunzo hayo kuleta ufanisi wa kazi zao za kila siku.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila amewataka viongozi na watendaji Mkoani humo kutumia mafunzo ya uongozi ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi za kila siku ikiwemo kutumia fedha za Serikali vizuri katika utekelezaji wa miradi mikubwa yenye tija kwa wananchi na kuchagiza maendeleo Nchini.
RC Chalamila ameyasema hayo leo Agosti 29, 2024 Kibaha, Mkoani Pwani wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya uongozi kwa viongozi na watendaji wa Mkoa wa Dar es salaam yanayofanyika kwenye Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere ambapo amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuimarisha utendaji na kuimarisha mahusiano kati ya viongozi, watendaji na wananchi
Aidha RC Chalamila amesema kupitia mafunzo hayo wanatarajia kuleta tija kubwa mojawapo kuongeza ufanisi wa kazi ambao utapelekea kuongeza mapato ya Mkoa lakini pia ,kutafsiri maono ya Mhe Rais kwenye kubuni miradi ya maendeleo pamoja na kuongeza fursa za uwekezaji jijini humo
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo ikiwemo Wakuu wa wilaya za Mkoa wa Dar es salaam, Mameya,Wakurugenzi Wakuu wa idara na Vitengo wamesema mafunzo hayo yataleta tija katika kuongeza uhusiano kati ya viongozi na wananchi pamoja na kuimarisha miradi ya maendeleo
Hata hivyo Katibu tawala wa Mkoa wa Dar es salaam Dkt Toba Nguvila ameeleza matarajio ya Serikali kwa viongozi hao baada ya kumalizika mafunzo hayo ikiwemo ukuaji wa uchumi na kuimarika kwa mahusiano kazini
Mwisho Mkoa wa Dar es salaam umeanzisha utaratibu wa kuwajengea uwezo viongozi na watendaji ikiwa ni kuongeza tija kwenye ushirikishwaji wa makundi yote muhimu kwenye shughuli za maendeleo