MKUU wa Mkoa wa Mara, Ally HApi akikagua mpaka wa Kirongwe amabo haujarasmishwa, wilayani Rorya Mkoa wa Mara. |
Ziara ya RC Hapi ilipoingia mpakani Kirongwe wilayani Rorya upande wa Kenya na kushuhudia jinsi jirani hao walivyojiandaa tayari kutoa huduma za mpakani. |
MRATIBU wa Mamlaka ya Forodha katika Kuzuia Magendo mkoani Mara, Robert Busungu (aliyevaa suti ya bluu) akielezea jinsi Mpaka wa Kirongwe kutorasmishwa kunavyoongeza magendo mkoani humo.
Na: Mwandishi wetu, MARA.
TOFAUTI ya bei za bidhaa mbalimbali kati ya Kenya na Tanzania imetajwa kuwa moja ya vyanzo vya kushamiri magendo mkoani Mara.
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara Ally Hapi alielezwa hayo na Mratibu wa Mpaka wa Sirari, Jackson Moshi akitaja Sementi, Sukari na Mafuta ya chakula kama mfano wa bidhaa ambazo bei zake Kenya ni nafuu ikilinganishwa na Tanzania.
“Mfano mfuko wa saruji (simenti) unapofikishwa mpakani upande wa Kenya unauzwa Sh 13,000(za kitanzania) wakati Simenti ambayo inazalishwa na viwanda vyetu ikifikishwa Sirari inauzwa kati ya Sh 22,000 hadi Sh 23,000,” alisema Moshi.
Kwa upande wa Mafuta ya chakula alisema Kenya lita 20 yanauzwa Sh 78,000 (Tz) wakati nchini yanauzwa Sh 82,000 na lita Tano kwa Kenya yanauzwa Sh 19,000 huku Tanzania yakiuzwa Sh 25,000 na kwamba hivi karibuni Mafuta yanayozalishwa Singida (Alizeti) yalipanda hadi kufikia Sh 39,000.
Hali hiyo inashawishi jamii kujihusisha na magendo, ingawa alisema wengi wanapata hasara kwasababu bidhaa nyingi zinakamatwa kwenye doria.
Alisema kwa sasa bidhaa zilizokamatwa ni pamoja na mifuko 605 ya Simenti 605, mifuko 130 ya Sukari na bidhaa nyingine ndogondogo za madukani.
Bidhaa hizo zimehifadhiwa muda siyo mrefu baada ya mifuko 1,200 ya Simenti kugawiwa kwa jamii na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, kwa kibali kilichotolewa na Kamishna wa Forodha nchini kama ambavyo utaratibu unaelekeza.
Akizungumzia mazingira ya mpaka huo kiusalama alisema kutoka kwenye Mpaka usiyo rasmi wa Kirongwe kuna umbali wa kilometa 78 ambapo kuna vipenyo visivyo rasmi 31 ambavyo vinaweza kuruhusu magari kupita.
Moshi alisema Kamishna wa Forodha aliunda timu ya kupambana na magendo, kufuatia kukithiri kwa vitendo hivyo mkoani Mara iliyoanza kazi rasmi mwezi mmoja uliyopita ikiratibiwa na yeye kwa kushirikiana na Mratibu wa Mkoa, Robert Busubu.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa huo, Samweli Kiboye alisema serikali inapoteza mapato kutokana na simenti inayoingizwa nchini kwa magendo.
“Mimi ni mtoto wa mjini hapa ninajua kwa siku mifuko ya simenti zaidi ya 1,000 inapitishwa, ukiangalia zilizokamatwa hazipungui Pikipiki 100 na kila moja inabeba siyo chini ya mifuko mitano, kuanzia Tarime mpaka Musoma wengi wanajenga kwa simenti ya magendo,” alisema Kiboye.
Alishauri Kamishna wa Forodha aweke utaratibu wa kutoza ushuru simenti inayoingizwa nchini, ili mapato ya serikali yapatikane na ikiwezekana bei ya bidhaa hiyo nchini iangaliwe upya ili iendane na uwezo wa wananchi.
RC Hapi anafanya ziara za kikazi mkoani humo ambapo alianza kwa kukagua miradi inayotekelezwa na Sekretarieti ya Ofisi yake kabla hajakagua Mradi wa Maji Shirati na mipaka ya Kirongwe na Sirari