ZANZIBAR.
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Mhe, Rahma Kassim Ali amewataka Walimu wakuu na Walimu wa TEHAMA kutovifungia katika makabati vifaa vya TEHAMA vilivyotolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) huku akiwaagiza kuhakikisha kuwa vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Waziri ameyasema hayo katika uzinduzi wa awamu ya tano ya mradi wa kugawa vifaa vya TEHAMA na kuziunganisha shule na mtandao wa intaneti (school connectivity), hafla ambayo imefanyika katika shule ya Sekondari ya Hasnuu Makame, Mkoa wa Kusini Unguja Visiwani humo.
Mhe, Rahma amesema, walimu wana wajibu wa kutunza na kuhakikisha kuwa vifaa hivyo vinatumika katika kujifunza na kufundishia ili kufikia malengo ya Serikali ya kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu ya TEHAMA kuanzia shuleni ili kuendana na kasi ya ukuaji wa sekta hiyo duniani.
Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Amour Hamil amesema, dhamira ya Serikali ni kuibadilisha Tanzania na kuifanya kuwa ya kidigitali kwa kuhakikisha kuwa mawasiliano na teknolojia ya habari yanasambaa katika maeneo yote ikiwamo maeneo ya vijijini na pembezoni.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadid ameishukuru UCSAF na kuongeza kuwa vifaa hivyo vitasaidia kukuza kiwango cha elimu ya TEHAMA katika Mkoa huo huku akiahidi kuwa atahakikisha vifaa hivyo vinatunzwa,vinaheshimiwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba amesema, awamu ya tano ya mradi huo imegharimu zaidi ya shilingi milioni 112 ikiwa ni manunuzi ya kompyuta 795 na printa 159 ambazo zitatolewa kwa shule 159 za Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo kila shule itapata kompyuta tano na printa moja. Ameongeza kuwa, Shule hizo pia zitaunganishwa na mtandao wa intaneti kwa lengo la kuwasaidia walimu na wanafunzi kutafuta taarifa mbalimbali zenye maudhui ya kieletroniki katika ufundishaji na kujifunza.
Amesema, UCSAF inawekeza kwa wanafunzi walioko shuleni kwa kuwapatia vifaa vya TEHAMA mapema ili wapate uelewa utakaisaidia nchi kuongeza idadi ya wataalam wa TEHAMA.
Nae Mkuu wa Idara ya Mawasiliano kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Clarence Ichwekeleza amesema kuwa ili kwenda sambamba na mabadiliko ya kiteknolojia duniani, Tanzania inahitaji vijana watakaokuwa na elimu na ujuzi zaidi wa TEHAMA.