Ofisa Habari kutoka Idara ya habari MAELEZO Beatrice Sanga akipokea kadi maalum ya utambulisho wa kupata chanjo kutoka kwa Ofisa wa zoezi hilo mara baada ya kuchanja katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam.
Na: Mwandishi wetu, DAR ES SALAAM.
Imeelezwa kuwa kutokana na Kazi za kuchangamana na jamii zinazofanywa na makundi ya wasanii, wanahabari na wanamichezo imepelekea makundi hayo kuweza kupewa kipaumbele ya kupata chanjo ya UVIKO – 19 kwa hiyari yao itakayowawezesha kufanya shughuli zao kwa uhuru huku wakiendelea kuchukua taadhali ya kujikinga na ugonjwa huo.
Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Matiko Mniko wakati wa zoezi la kutoa Chanjo kwa hiyari kwa Makundi maluum ya Wasanii, wanamichezo na Wanahabari lililofanyika leo katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam, ambapo amesemakuwa makundi hayo mara nyingi kazi zao zimekuwa zikijihusisha na kuchangamana na jamii hivyo Serikali imeona ni vema kuwapa kipaumbele cha kupata chanjo hiyo kwa hiyari yao.
Amesema kuwa licha ya Serikali kutoa miongozo mbalimbali ya kujikinga na ugonjwa huo ikiwemo kuvaa Barakoa, kunawa mikona kwa maji tiririka na kutumia vitakasa mikono lakini imeona haitoshi kwa maana hatari bado iko palepale ndio maana imeona ni Muhimu kwa wadau hao kupata chanjo kwasababu kazi zao ni zakuchanagamana sana
”Tumpongeze sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu hasaani kwa kukona umuhimu wa Makundi haya kupata chanjo kwa hiyari yao ili waweze kufanya shughuli zao za ujenzi wa Taifa kwa maana hiyo sasa leo pamoja na kesho imeona iwape kipaumbele makundi haya kuweza kupata chanjo” Amesema Mniko.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Tanzania Chiki Mchoma amesema kuwa mwitikio wa Wasanii umekuwa mkubwa na wamejitokeza kwa wingi kwenye zoezi hilo na kwamba anaishukuru Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kuweza kuyakumbuka makundi hayo na kuwapatia chanjo hiyo.
“Sisi tunaipongeza sana Serikali kupitia wizara chini ya kaka yetu Mheshimiwa Waziri Bashungwa kuweza kutufikiria na kuona umuhimu wa sisi kwa umoja wetu kuwepo hapa kwaajili ya kupata chanjo, lakini pia tunamshukuru sana ndugu yetu Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbas ambaye kimsingi amefanya kazi kubwa ya kutuonesha umuhimu wa sisi kupata chanjo kutokana na shughuli zetu” Amesema Chiki.
Nae Mwandishi wa Habari Mwandamizi Saidi Kengele amesema kuwa umuhimu wa kupata chanjo hiyo sio kwa wanahabari, wasanii, na wanamichezo peke yao ila wananchi wote waone umuhimu wa kupata chanjo hiyo kwani Serikali yao imewajali sana ili kuweza kufanya kazi na kujenga Taifa kwa ujumla.
Zoezi hilo la kuwapatia Chanjo makundi hayo maalum ya Wasanii, Wanahabari na Wanamichezo limefanyika leo kufuatia tangazo lililotolewa na katibu mkuu wa wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Hassan Abbas hivi karibuni.