Na: Mwandishi Wetu,TARIME.
MHANDISI wa Halmashauri ya Tarime, Eng. Ernest Maungo Leo amewekwa rumande na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Tarime, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi kubaini madudu kwenye Mradi wa Ujenzi wa Bwalo la Shule ya Sekondari ya Manga iliyopo Kijiji cha Surubu Kata ya Komaso.
Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Editha Nakei amesema gharama ya mradi huo ni zaidi ya Sh milioni 100 na kwamba mpaka ulipofikia umetumia Sh milioni 96.4.
Hata hivyo RC Hapi baada ya kushuhudia jinsi nguzo za jengo hilo zilivyopinda na kuta zake kuinama, ameamuru livunjwe haraka ili kuepusha hatari inayoweza kutokea endapo litaanguka.
Pia ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kukamata na kuhoji kila aliyehusika na mradi huo, ili atakayethibitika kuhusika na ‘kutupa jalalani‘ fedha hizo za serikali azirudishe.
Bodi ya Shule hiyo pia imevunjwa na Mkuu wa Mkoa Hapi ambaye ametaka kila mjumbe ahojiwe na TAKUKURU na kwamba anaweza kuamua vinginevyo baada ya uchunguzi kukamilika.
Akizungimza nasi katika mahojiano maalumu, Mkuu wa TAKUKURU wa Mkoa wa Mara, Hassan Mossi hakukanusha wala kukiri kuagiza kukamatwa Eng. Maungo, ingawa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime, RPC William Mkonda amethibitisha kuwa wanaye.
Mkuu Mossi amesema baadhi ya miradi ukiwemo wa Jengo hilo walishaanza kuifanyia kazi na uchunguzi upo kwenye hatua ambazo siyo sahihi kwao kuzizungumzia kwenye vyombo vya habari.
“Wakati wa kutoa taarifa kwa umma ukiwadia, tutafanya hivyo nina hakika mnafahamu kuwa hii ni taasisi ya uchunguzi,”amesema Mossi.
Naye Afisa Elimu – Sekondari wa Halmashauri hiyo, Victor Emmanuel akizungumza nadi katika mahojiano maalumu amesema endapo ujenzi huo ungekamilika jengo lingehudumia watu 400.