Na. MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya Classic Finishes Limited ambayo inafahamika zaidi kwa jina la Mkeka wa Mbao, imezindua bidhaa mpya ya Firmfit (sakafu) huku ikisisitiza bidhaa hiyo ni rafiki kwa uchumi na mazingira.
Mkurugenzi Mkuu wa Classic Finishes Limited, Eda Sylvester akizungumza katika hafla katika uzinduzi wa ushirikiano kati ya Classic Finishes Limited na Kampuni ya Creative Flooring Solution (CFL), pamoja na uzinduzi wa bidhaa ya firmfit ambayo inapatikana Afrika nzima kupitia Classic Finishes Limited, jijini Dar es Salaam, leo, amesema kuwa bidhaa zao zinazingatia ubora kulingana na wakati na hali za uchumi wa wananchi.
Eda ameeleza kuwa Classic Finishes Limited inauzoefu wa kutoka katika bidhaa za kupamba nyumba hususan kuta na sakafu na siku zote wamekuwa wakizingatia ubunifu na ubora wa bidhaa.
“Classic Finishes Limited ilianzishwa mwaka 2019 kwa kuwa na bidhaa moja ya BELKA mahususi kwa kupamba kuta. Kuanzia hapo safari yetu inaendelea kukuwa na kuzingatia ubunifu. Kwa miaka mitano iliyopita tumeongeza bidhaa mbalimbali.
“Miongoni mwa bidhaa hizo zipo 10 ambazo kwa zaidi ya asilimia 80 tumeshirikiana na Kampuni ya Creative Flooring Solution (CFL) ambayo inafanya shughuli zake katika nchi za Ubelgiji, Uingereza, Marekani, China na Vietnam. Malengo yetu ni kuwa kampuni kiongozi kwa bidhaa za kupamba kuta na sakafu Tanzania na Afrika kwa ujumla,” alisisitiza.
Alieleza kutokana na malengo hayo wamekuwa wakitafuta washirika sahihi kufanikisha safari ya kuongeza ubora na ubunifu ndio ambapo amefafanua Januari mwaka huu walishiriki maonesho ya kibiashara ya Domotex na kufanikiwa kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa juu wa CFL Rais wake Thomas Baert pamoja na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Tom Van Poyer ambayo yamezaa ushirikiano.
Ameeleza kuwa ushirikiano huo umezinduliwa rasmi leo na kushuhudiwa na wadau mbalimbali wakiongozwa na Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Baraka Eligaeshi aliyemwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.
Eda aliishukuru serikali na kumpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kufungua milango ya uwekezaji kwa wazawa na wageni hatua ambayo inachochea mafanikio yao.
Akizungumza katika hafla hiyo, Eligaeshi amewataka wadau wa uwekezaji nchini kufungua fursa zaidi katika uwekezaji kwa kuingia ubia na wafanyabiashara wa kimataifa lengo ni kukuza uchumi na kuongeza wigo wa kibiashara.
Pia, ameipongeza Classic Finishes Limited kwa kuingia mkataba huo wa kimataifa unaotengeneza mazingira mazuri kwa taifa kukuwa kiuchumi na maendeleo endelevu huku akisisitiza bidhaa zinazozalishwa na kampuni hiyo ni rafiki kwa mazingira na uchumi.
“Kupitia ushirikiano huu tunatarajia kuona uvumbuzi zaidi wa bidhaa zitakazoleta ushindani katika soko la ndani na kimataifa. Sekta ya ujenzi na miundombinu kwa kipindi cha miaka 10 imechangia asilimia 15 ya pato la taifa (GDP), hivyo mnapaswa kuelewa kuwa mmewekeza katika sekta muhimu na sahihi kwa maendeleo,” amesema.
Wakati huo huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa CFL, Tom Van Poyer amesema wamevutiwa kushirikiana na Classic Finishes Limited kwa kuwa ni kampuni sahihi kwa mkakati wao wa kujitanua kibiashara katika soko la Afrika.
#Classic_finishestz
#mkeka-wa- mbao-original