Na Richard Mwamakafu – WHUSM, Dodoma
Shirikisho la Mpira wa Miguu wa Barani Afrika (CAF) chini ya Rais wake Paracti Motsepe imevutiwa na jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza michezo nchini hususan Soka.
Miongoni mwa jitihada zilizovutia Shirikisho hilo zinachukuliwa na Serikali katika kuendeleza michezo nchini ni pamoja na kuondolewa VAT kwenye nyasi bandia ili kuboresha miundombinu ya michezo nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa mara baada mkutano wa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa alipotembelewa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) Paracti Motsepe na kufanya naye mazungumzo leo Agosti 13, 2021 Jijini Dodoma.
Jitihada nyingine zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha michezo nchini ni kutunisha Mfuko wa Maendeleo ya Michezo unaosimamiwa na Baraza la Michezo nchini (BMT), mkakati wa kurudisha uhai wa michezo katika shule za msingi (UMITASHUMTA) pamoja na shule za Sekondari (UMISETA) ambayo Rais huyo amefuatilia kwa karibu mashindano ya mwaka huu yaliyofanyika kitaifa mkoani Mtwara.
Katika majadiliano yao na Waziri Mkuu Majaliwa, wamekubaliana kuhakikisha vipaji vinavyopatikana katika shule hizo vinaendelezwa pamoja na kuboresha miundombinu ya michezo nchini.
Adha, Waziri Bashungwa amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha na kuendeleza sekta ya Michezo na Utalii nchini ambapo Mkutano Mkuu wa CAF unatarajiwa kufanyika nchini unaoshirikisha Marais 54 wa Mpira katika nchi mbalimbali Barani Afrika pamoja na ujumbe wao wanatarajiwa kushiriki na baada ya mkutano wao watapata fursa ya kutembelea Hifadhi za Taifa na maeneo mengine ya yenye vivutio vya utalii. Hiyo ni fursa adhimu kwa taifa katika kuendeleza utalii wa michezo ambayo inatatoa mchango mkuwa katika uchumi wa mtu mmoja mmoja na kuongeza pato la taifa kwa ujumla.