Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu, akizungumza katika kikao kazi na Wahariri wa vyombo vya habari kilichofanyika leo Julai 15 Jijini Dar es salaam.
Na; Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kikao kazi cha wenyeviti wa Bodi na watendaji wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali kitakachofanyika mwezi Agosti mwaka huu Jijini Arusha.
Hayo yameelezwa na Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu, katika kikao kazi na Wahariri wa vyombo vya habari kilichofanyika leo Julai 15 Jijini Dar es salaam, ambapo amesema kuwa kikao hicho kitafanyika katika kituo cha kimataifa cha mikutano Arusha (AICC), na kitabebwa na kaulimbiu isemayo ‘ Mikakati ya Taasisi na Mashirika ya Umma Kuwekeza Nje ya Tanzania’.
‘Kikao kazi hicho kitalenga kwenda kuhimiza Taasisi na mashirika ya umma kuangalia zaidi fursa za kuwekeza au kupanua wigo wa huduma nje ya Tanzania’ amesema.
Aidha Mchechu ameongeza kuwa kuna maeneo muhimu ya kufanyiakazi katika kikao kazi hiko ambacho ni cha pili kufanyika, na kuongeza kuwa kikao hicho kitapitia hatua zinazofanywa katika utendaji wa maazimio yaliyofikiwa kwenye kikao kazi kilichopita mwaka 2023.
Pia, ameongeza kuwa kikao hicho kitajadili fursa za kikanda na kimataifa kwaajili ya Taasisi na Mashirika kuwekeza nje ya nchi sambamba na kupata uzoefu wa kiutendaji kazi kutoka kwa wataalamu wa ndani na nje ya nchi.
“Uboreshahi wa mitaji ya Mashirika haya ni kupelekea ujuzi na utendaji kazi katika ushindani, na kuweza kubadilisha mitazamo na kufanya Taasisi na Mashirika hayo kuwa vichocheo vya maendeleo ya kiuchumi.
‘Tunatakiwa kukumbuka mambo muhimu ambayo Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wanapaswa kuzingatia katika usimamizi wa utendaji kazi ikiwemo Miongozo mbalimbali ya Uendeshaji wa Mashirika ya Umma pamoja na umuhimu wake katika kutekeleza malengo ya Serikali kwa ufanisi” ameongeza Mchechu.
Amesema anaamini kikao hicho kinakwenda kutatua changamoto zilizopo katika uendeshaji wa Taasisi na kuweza kuainisha mikakati iliyopo, pia taasisi zinazofanya vizuri katika nyanja mbalimbali za utendaji kazi zikiwemo kutengeneza faida na kufanya mageuzi ya utendaji na kuboresha utoaji wa huduma zitatambuliwa na kupewa tuzo.
Mwisho.