MKURUGENZI wa Kampuni ya Gomzoe Neema Ngowi mbayo imejikita kwenye kilimo cha Piliili Manga pamoja aina mbalimbali za viungo ambazo wanazipata kwa wakulima kama malighafi na kuzichakata amewaomba wananchi wanaotembelea Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba kufika kwenye banda lao ili kupata huduma za bidhaa walizonazo sambamba na Asali yenye ladha tofauti baada ya kuchanganywa na viungo.
Akizungumza katika mahojiano maalum Julai 3, 2022 akiwa katika Banda la Mama Anna Mkapa, amesema wamekuwa wakitengeneza viungo vya aina mbalimbali ambavyo vinatokana na mbegu asilia hivyo watu wengi kuvutiwa na sasa wapo katika Maonesho hayo kwa ajili ya kuuza bidhaa zao.
“Kampuni yetu kwa sehemu kubwa tunajishughulisha na kilimo cha Pilipili Manga lakini tumekuwa tukinunua viungo vya aina mbalimbali kutoka kwa wakulima wenzetu ambavyo tunazichakata na kupata viungo kama Masala. Pia tunavyo viungo ambavyo vinajitegemea tunaweza kusema single single.
“Pia tuna asali mbichi pamoja na asali ya nyuki wadogo, asali zetu ziko tofauti kwasababu zimeungwa, kuna asali ambayo iko na Jinja ,tangawizi na kuna asali ambayo iko na manjano. Asali hizi ni maalum kabisa kwa ajili ya tiba ya mfuko wa hewa ,tunawakaribisha muweze kuona na kupata huduma kama hii kutoka kwetu,”amesema Ngowi.
Kuhusu Maonesho ya Sabasaba ,Ngowi amesema huu ni msimu wake wa tatu kushiriki na kwa mara ya kwanza akishiriki kupitia Chama kinachojihusisha na viungo (Spaces) na kuhusisha wadau wote na mwaka huu ameshiriki kupitia mwamvuli wa Taasisi ya Mama Anna Mkapa. “Mama Mkapa kupitia taasisi yake amekuwa akituwezesha wajasiriamali kutuinua kichumi kwa maana ya kuondokana na umasikini. Na shughuli zangu kwa ujumla niko pale Kijiji cha Makumbusho kwa maana ya eneo la kuuzia, lakini kwa upande wa uchakataji na ufungaji bidhaa niko Bunju.”
Akizungumzia Maonesho ya mwaka huu wa 2022 amesema yako kitofauti kwasababu Watanzania wamekuwa na mwanga zaidi hata ukiangalia ufungashaji wa bidhaa zao na upangaji wa bidhaa muonekano ni mzuri.
“Kama unavyokumbuka katika kipindi cha miaka miwili tulikuwa na changamoto ya COVID-19 lakini hata hivyo Mungu aliweza kutusaidia tukaweza kushiriki ila mwaka huu wa 2022 Mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan kama ametufungulia Dunia. Tunatembelewa na wageni mbalimbali.
“Wageni hao wamekuwa wakiuliza bidhaaa zetu na wanazipenda kwasababu ni bidhaa asilia ,hakuna bidhaa ambayo inatokana na mbegu za maabara, ni mbegu asili. Kwa hiyo wanafurahia sana,”amesema wakati akielezea Maonesho hayo.
Kuhusu Taasisi ya Mama ana Mkapa amesema kuwa ni taasisi bora kabisa ,hivyo anawashauri wanawake wenzake wote ambao wanajishughulisha waweze kutafuta nafasi ya kukutana na Taasisi hiyo au uongozi wake ili kuweza kushiriki pamoja nao.
Ameongeza kumekuwa na mafunzo mbalimbali yanayotolewa yanayoweza kuwafanya wapige hatua. “Ukija katika taasisi hi huwezi kufanana na pale ulikokuwa,ni lazima utatoka pale na kuelekea upande wa pili ,ukweli tunaondokana na umasikini kwasababu tunaona mabadiliko,ushindani ni mkubwa kwani tuko wanawake kutoka mikoa mbalimbali ,hivyo unaona wenzako wanavyofanya lakini inakuwa ni sehemu ya wewe kumjua mwenzako na kupata soko la kuweza kupata malighafi kutoka kwao , kwa hiyo nawakaribisha sana wanawake wenzangu tuweze kushiriki.
Mama namba moja sijui niseme nini nampenda kumpa salamu.kipekee kama Mwanamke ambaye amenifanya niendelee kuwa jasiri, kuwa tofauti kabisa katika jamii kuweza kuwaamsha wanawake wenzangu kujishughulisha ,napenda kuwaambia wanawake wenzangu waamke,watazame vile Mwanamke anaweza kuongoza Jeshi kubwa sio tu kwa Tanzania tazama kama Afrika Mashariki kote anaweza kushirikiana nao katika kuleta maendelo lakini ameweza kuifungua nchi na Dunia amefanya tuonekane na sisi kupata fursa mbalimbali kwa hiyo ninapenda kuchukua nafasi hii kumshukuru mama namba moja muheshimiwa madame Rais.