Na Georgina Misama, CBE, Dar es salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dk. Hashil Abdallah amewataka Watanzania hususan wafanyabiashara kutumia tafiti zinazofanywa na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) ili kuboresha huduma zao.
Dk. Abdallah amesema hayo leo Julai 13, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akitoa hotuba yake katika hafla ya uzinduzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Miaka Sitini (60) ya CBE zilizofanyika katika Kampasi kuu ya Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Chuo hicho Prof. Edda Tandi Lwoga.
Alisema tafiti zinazofanywa na CBE zitaendea kutumiwa na Serikali katika kuboresha Sera na Mikakati ya Viwanda na Biashara nchini na kwamba zikitumiwa vizuri na makampuni binafsi zitasaidia kuboresha bidhaa zao na kuongeza ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Tunaitaka CBE iendelee kutoa mafunzo na tafiti zinazolenga kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya Viwanda na Biashara nchini, aidha, nawapongeza kwa juhudi zenu kwa kuhakikisha Chuo kinaendelea kuwa kinara katika kutoa elimu ya biashara nchini,” alisema Dk. Abdallah.
Awali, Mkuu wa Chuo, Prof. Edda Tandi Lwoga, alielezea historia na mafanikio ya CBE tangu kuanzishwa kwake mwaka 1965 na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alisema CBE inajivunia kuwa na kampasi nne nchini na kutoa elimu bora kwa wanafunzi zaidi ya 19,000.
Alisema CBE imepanua programu zake kutoka 1 kilipozinduliwa hadi zaidi ya 22 mwaka 2024, ikijumuisha Biashara, Uhasibu, Masoko, Manunuzi na Ugavi, TEHAMA, na nyinginezo, vile vile Prof. Tandi alitambulisha Dira ya miaka 50 ya CBE, “CBE Vision 2074,” inayolenga maendeleo endelevu kupitia teknolojia mpya na tafiti za kina.