Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na Guinea-Bissau zimekubaliana kukuza ushirikiano na uhusiano katika sekta mbalimbali.
Rais Samia amesema hayo leo wakati yeye na mgeni wake Rais wa Guinea-Bissau Mhe. Umaro Sissoco Embaló walipokuwa wakizungumza na vyombo vya habari katika hafla iliyofanyika Ikulu wakati wa ziara ya Rais huyo.
Awali katika mazungumzo yao, Marais hao wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kuendeleza uzalishaji wa zao la korosho hasa kupitia tafiti ili kuweza kuimarisha mnyonyoro mzima wa thamani wa zao hilo ikiwemo kuanzisha vyama vya ushirikiano ili kukuza zao na bei ya zao hilo katika soko la dunia.
Masuala mengine waliojadiliana ni pamoja na kukuza biashara na uwekezaji ikiwemo kuimarisha ushirikiano kwenye sekta za uchumi wa buluu, sekta za afya, elimu, ulinzi na usalama pamoja na masuala ya kimataifa.
Rais Samia pia amesema ziara ya Rais Embaló imefungua upya milango ya ushirikiano na mahusiano.
Rais Samia ameyasema hayo baada ya kushuhudia utiaji saini mkataba wa mwongozo wa ushirikiano ambao utaimarisha zaidi ushirikiano uliopo kwa manufaa ya nchi hizo mbili na wananchi wake.
Kwa upande wake Rais Embaló ametambua na kushukuru mchango wa Tanzania kwenye ukombozi wa bara la Afrika ikiwemo Guinea-Bissau.
Rais huyo pia alitumia fursa hiyo kumualika Rais Samia kufanya ziara nchini humo.
Aidha, Rais Embaló amewakaribisha wadau wa sekta binafsi nchini kutumia Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) kuwekeza nchini Guinea-Bissau na kutumia nchi hiyo kama lango la kukuza biashara na ukanda wa Afrika Magharib.
Sharifa B. NyangaKaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu