Home BUSINESS FCC YAZINDUA MAADHIMISHO YA KITAIFA SIKU YA USHINDANI DUNIANI

FCC YAZINDUA MAADHIMISHO YA KITAIFA SIKU YA USHINDANI DUNIANI

NA Mwandishi wetu, DAR

Tume ya Ushindani (FCC) imedhamiria kutoa elimu kwa Watanzania juu ya namna nzuri ya kufanya biashara pasina kudidimiza sera na taratibu za ushindani za ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa FCC William Erio siku ya Ijumaa Novemba 29, 2024 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za taasisi hiyo mkoani Dar es Salaam, ambapo FCC imezindua Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Ushindani Duniani ambayo kilele chake kitakuwa tarehe 8 Desemba, 2024.

Amesema ili kufanyika kwa biashara katika mazingira ya haki na usawa, ni muhimu kuwa na udhibiti kupitia sera na sheria akitolea mfano mikataba yote inayokinza na ushindani, na miungano yote ya kampuni ambayo inafifisha ushindani.

Hata hivyo Erio amesema kuwa licha ya nchi kuwa na misingi ya biashara huria, kuna utofauti wa rasilimali kutoka kwa wafanyabiashara ambapo wakifanya biashara katika misingi hiyo bila utaratibu wa aina yoyote, watu au kampuni zitaumia kwa kushindwa kupata fursa sawa ya kufanya biashara.

“Kuna mbinu nyingi chafu zinaweza kutumika kwenye utendaji wa biashara, mfano wafanyabiashara kuwaondoa washindani wao sokoni ili wabaki peke yao, kwasababu mfanyabiashara yeyote lengo lake ni kupata faida, sasa mkiwa wengi faida itapungua ingawa ufanisi na upatikanaji wa bidhaa utaongezeka, kwahiyo anaweza kuamua kwa makusudi kabisa kufanya vitu ambavyo vinafifisha ushindani na kwa nguvu yake aliyonayo aidha ya kifedha, rasilimali watu au utaalamu akawasababisha wengine wakashindwa kufanya biashara sokoni na kuondoka”, ameeleza.

Amesema changamoto zote hizo zinatokana na kutokuwa na usawa kwa wafanyabiashara hao hivyo amesema kama taasisi jukumu la FCC ni kutengeneza mazingira sawia ya watu wote kufanya biashara kwa usawa kupitia sera na sheria.

Kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika tarehe 5 Disemba 2024 katika Hoteli ya Golden Tulip, Oysterbay, Dar es Salaam ambapo Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi. Kilele hicho kitaambatana na kongamano litakalowakutanisha magwiji wa sheria na biashara ambao watajadili mazingira ya biashara na ushindani Tanzania na watapata fursa ya kuishauri FCC juu ya namna nzuri ya kutekeleza majukumu yake.

Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Ushindani Duniani, kaulimbiu ‘Sera ya Ushindani na Kudhibiti Kukosekana kwa Usawa katika Uchumi’.

Previous articlePRESIDENT NGUEMA, 2024 LAURANTE OF THE BABACAR NDIAYE TROPHY, TO HOST THE FIRST SUMMIT OF AFRICA’S GREAT BUILDERS
Next articleHAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMAMOSI TAREHE 30, NOVEMBA -2024
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here