Home LOCAL RAIS SAMIA ARIDHIA OMBI LA MSAJILI WA HAZINA KUTENGA SIKU MAALUM YA...

RAIS SAMIA ARIDHIA OMBI LA MSAJILI WA HAZINA KUTENGA SIKU MAALUM YA KUTOA GAWIO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia Viongozi wa Serikali, Wakuu wa Mashirika na Taasisi za Umma pamoja na wageni mbalimbali mara baada ya kupokea Gawio na Michango kutoka kwa Mashirika na Taasisi hizo, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 11 Juni, 2024.

DAR ES SALAAM 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameridhia ombi la Msajili wa Hazina Mhe. Nehemia Mchechu la kutenga siku maalum kila mwaka na kuwa siku ya Mashirika na Taasisi za Umma kutoa gawio kwa Serikali.

Rais Samia ameyasema hayo leo wakati akihutubia kwenye hafla ya Taasisi na Mashirika ya Umma kutoa gawio na michango kwa Serikali iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Aidha, Rais Samia amesema Serikali inaweka mazingira bora ya kufanya biashara, kutunga sera rafiki zinazohamasisha uwekezaji nchini kwa nia ya kuimarisha uchumi na kuboresha huduma za jamii.

Vilevile, Rais Samia amesema upokeaji gawio ni ishara kuwa mazingira yaliyowekwa yanafanya kazi na kuwezesha kupatikana kwa fursa ya kufanya biashara na kupata faida. Rais Samia pia ametoa wito kwa viongozi wa Mashirika yote ambayo bado hayajatoa mchango wake kwa Serikali, na yale ambayo yametoa chini ya kiwango wanachotakiwa kutoa, kuhakikisha wanafanya hivyo kabla ya Mwaka wa Fedha wa 2024 haujaisha.

Hali kadhalika, Rais Samia amesema kuwa ataendelea kusimamia mageuzi katika uendeshaji wa Mashirika ya Umma ili kuyawezesha kujiendesha kibiashara na kwa tija zaidi kwa manufaa ya Watanzania.

Rais Samia ameelekeza Mashirika kufikia mwezi Desemba 2024 kuhakikisha mifumo ya Serikali inasomana kama walivyofanya Shirika la Mapato nchini (TRA) na Mamlaka ya Bandari (TPA).

Katika hafla hiyo, Rais Samia amepokea gawio na michango kutoka kwa mashirika 145 yenye thamani ya jumla ya Shilingi 637,122,914,887.59 ikijumuisha gawio Shilingi 278,868,961,122.85 kutoka katika Mashirika ya Biashara na michango Shilingi 358,253,953,764.74 kutoka katika Taasisi nyingine.

Sharifa B. NyangaKaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu

Previous articleRAIS DKT. SAMIA AHUTUBIA MARA BAADA YA KUPOKEA GAWIO NA MICHANGO KUTOKA MASHIRIKA NA TAASISI ZA UMMA, IKULU JIJINI DAR ES SALAAM
Next articleTASAC YACHANGIA GAWIO LA BILIONI 19.1 KATIKA MFUKO WA HAZINA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here