Home BUSINESS NIMEIACHA CBE KATIKA MIKONO SALAMA: Prof. ANDERSON 

NIMEIACHA CBE KATIKA MIKONO SALAMA: Prof. ANDERSON 

Na: Georgina Misama, CBE.

Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof. Wineaster Anderson amesema anaondoka katika nafasi hiyo akimshukuru kila mmoja uongozi wa chuo, wafanyakazi na wanafunzi wa chuo hicho na kwamba amekiacha chuo katika mikono salama.

Prof. Wineaster amesema hayo leo Juni 6, 2024 katika hafla fupi ya kuwaaga wajumbe wa bodi hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam baada ya kuhudumu kwa miaka mitatu, ambapo alisema alianza kuiongoza bodi hiyo mwaka 2018 na kwamba amehudumu kwa vipindi viwili hivyo ameshuhudia maendeleo mengi ya chuo hicho.

“Tumpongeze sana Mkuu wa chuo Prof. Edda Tandi Lwoga kwa uongozi wake, amekuwa kiongozi mahiri ninaondoka nikijua chuo nimekiacha katika mikono salama, Prof. Tandi anafanya kazi yake vizuri sina mashaka nae, lakini pia naushukuru uongozi na kila mwanajumuia ya CBE, hiki ni chuo ambacho kinawapenda wafanyakazi wake,” alisema Prof. Anderson.

Awali akitoa neno la utangulizi Mkuu wa chuo cha CBE Prof. Edda Tandi Lwoga aliishukuru bodi hiyo kwa kazi kubwa iliyofanya katika kipindi chake na kwamba ameshuhudia chuo hicho kikipiga hatua za maendeleo ikiwemo uwezo wa kuandaa Dira ya Miaka 50 ya chuo hicho ikiwa ni tukio la kihistoria.

“Kwa mara ya kwanza tunaenda kuiangalia CBE kwa miaka 50 ijayo, ni jambo la kihistoria kwetu, lakini pia katika kipindi cha bodi hii wameweza kusimamia ujenzi wa kampasi yetu ya Mbeya ambapo hivi sasa tumeweza kuhamia katika majengo yetu wenyewe,” alisema Prof. Lwoga.

Vilevile alisema katika kipindi cha bodi hiyo, chuo kimeweza kuandaa wazo la kutafuta mwekezaji ili kuweza kutengeneza vyanzo vya fedha, aidha, Prof. Lwoga aliahidi kuendeleza ushirikiano na wajumbe hao wa bodi hata watakapokuwa nje ya jukumu hilo.

Kwa upande wake Naibu Mkuu wa Chuo hicho anayeshughulikia Fedha, Mipango na Utawala Prof. Emmanuel Munishi aliwashukuru wajumbe wa bodi waliomaliza muda wao kwa kusimamia misingi ya uongozi na kwamba katika kipindi chao amejifunza mambo mengi.

“Uongozi wenu haukuishia tu kufuata sheria, taratibu, kanuni na miongozo bali mlitufanya sisi pia kujifunza uongozi kwenu, yale mliyotuanzishia tutayaendeleza kwani tumepata michango mbalimbali kutokana na ujuzi wa kila mmoja wenu tunawashukuru kwa ahadi yenu ya kuendelea kushirikiana nasi, mtaendelea kuwa sehemu ya familia yetu”, alisema Prof. Munishi.

MWISHO

Previous articleBARRICK YAADHIMISHA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI 2024 KWA VITENDO
Next articleSOMA NAGAZETI YA LEO IJUMAA JUNI 7-2024
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here