MBEYA
Chemba ya Biashara,Viwanda na Kilimo imetakiwa kuongeza wigo wa washiriki wa maonesho ya biashara Mbeya City Expo msimu ujao kwa kuwaalika wafanyabiasha kutoka nchi za Malawi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tofauti na sasa wanavyoalika mabalozi wa nchi hizo pekee.
Akizungumza wakati wa kufungua Maonesho ya Biashara Mbeya City Expo 2024, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera ambaye amemuwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji amesema, kufanya hivyo kutasaidia kuziona bidhaa mbalimbali na kujifunza jinsi ambavyo wafanyabiashara wa mataifa mengine wanavyoandaa na kudumisha ubora wa bidhaa zao.
Mkuu huyo wa Mkoa ameongeza kuwa faida nyingine ya kuja kwa wafanyabiashara kutoka kwenye mataifa hayo ni kutengeneza mfumo ambao utawezesha wafanyabiasha wa Tanzania kwenda kwenye nchi hizo kuonesha bidhaa zao na kutanua wigo wa soko utakaoboresha kipato chao na pato la Taifa.
Aidha Mhe. Homera amewataka wadau wa biashara kuzitumia fursa zilizopo Mkoa wa Mbeya ikiwemo miundombinu ya usafiri majini upande wa ziwa Nyasa, usafiri wa anga uwanja wa ndege wa kimataifa Songwe kwakuwa hivi sasa zinafanyika safari za usiku, barabara ya njia nne ambayo imeanza kujengwa sambamba na reli ya TAZARA ambayo Serikali imepanga kuiboresha ili kurahisisha usafirshaji wa mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam kuja kwenye mikoa ya nyanda za juu kusini na nchi jirani za Malawi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kwa upande wake Rais wa TCCIA Bw. Vicent Minja amesema kuwa miaka mitatu ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, kumekuwa na mabadiliko makubwa katika sekta ya uwekezaji na uchumi ambapo kituo cha uwekezaji kimerekodi miradi mipya zaidi ya 1188 ambalo ni ongezeko la asilimia 63.19 ikilinganishwa na miaka mitatu iliyopita.
Bw. Minja ameeleza kuwa kulingana na kasi ya Serikali ya awamu ya sita, inaifanya TCCIA kuongeza kasi ya uboreshaji wa huduma katika sekta hizo ili kufikia malengo ya pamoja kwa ajili ya kuimarisha uwekezaji na uchumi nchini.
Naye, Mkurugenzi msaidizi wa Maendeleo ya Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Bi. Crestencia Mwimbwa ametoa wito kwa wadau wanaoshiriki maonesho ya MBEYA CITY EXPO 2024 kujifunza juu ya biashara zinazopatikana katika maonesho hayo na kuzitumia vyema fursa adhimu za tukio hilo.
Maonesho ya Mbeya City Expo mwaka huu ni ya pili kufanyika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023 yakiwa ni maono ya TCCIA na Serikali ya Mkoa wa Mbeya na kuyafanya kuwa maonesho makubwa ya kimataifa kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.