Peter Haule, WF, Dodoma
Serikali imesema kuwa imeunda kamati ya kukusanya na kuchambua maoni na mapendekezo ya viwango vya nyongeza ya pensheni ili kuwezesha maandalizi ya rasimu ya Waraka wa Baraza la Mawaziri kuhusu nyongeza ya pensheni kwa wastaafu wanaolipwa na Hazina.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Taska Restituta Mbogo, aliyetaka kufahamu lini Serikali itawaongezea pesheni wastaafu wanaolipwa shilingi 100,000 kwa mwezi na Hazina.
Alisema kuwa Kazi ya uchambuzi wa maoni na mapendekezo ya wadau kuhusu mapendekezo ya viwango vya nyongeza ya pensheni inatarajiwa kukamilika kabla ya tarehe 30 June 2024.
Aidha kuhusu fomula ya kikokotoo, Dkt. Nchemba alisema kuwa  Kamati imeundwa na inahusisha watu mbalimbali na Wizara inayohusika na utumishi nayo inaendelea na zoezi kubwa linalohusisha masuala ya pensheni kwa ujumla wake.
Akizungumzia mafunzo kwa wastaafu wanaolipwa na Hazina kabla ya kustaafu, alisema kuwa mafunzo yanaendelea kutolewa na yataboreshwa ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma hiyo.