Na: Halfan Abdulkadir- Zanzibar
Wadau wanaopinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia Zanzibar ,wametakiwa kuendelea kuelimisha jamii juu ya masuala ya malezi kwa watoto ili watambue haki na wajibu kuhusu afya ya uzazi
Mkuu wa Divisheni ya Watoto Mohammed Jabir Makame ameyasema hayo katika kikao cha siku moja cha kupitia muongozo wa malezi na Mawasiliano kwa vijana baleghe kilichofanyika katika ukumbi wa kituo cha Walimu TC Kiembe Samaki Mkoa wa Mjini Magharib Unguja.
Ndugu Mohammed amesema bado wazazi wana changamoto ya kutozungumza na watoto wao namna bora ya kujihifadhi na kujilinda juu ya afya ya uzazi hali inayopelekea kutokea mimba za umri mdogo.
“Ni vyema ulivyotengenezwa huo muongozo kwani utasaidia sana jamiii kuleta mabadiliko pindi ukikamilika,” alisema
Naye Afisa Elimu na Afya Katika Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu Sayansi na Utamaduni UNESCO Hasina Salim Bukheti, amesema wameandaa muongozo huo ili kusaidia mawasiliano baina ya mzazi na mtoto kuzungumza pamoja masuala ya afya ya uzazi.
Amesema muongozo huo unaendeshwa nchi za Afrika Mashariki na Kusini na wameufanya uwe rafiki kuendana na mazingira na tamaduni za nchi husika.
Amesema katika tafiti zao mbalimbali wamebaini kuwa wazazi na watoto wa Zanzibar hawazungumzi masuala ya uzazi hivyo huwapa mwanya mpana wa kushindwa kuelewana kwenye eneo hilo.
“Tunaamini kupitia muongozo huu, utarahisisha mawasiliano kati ya mzazi na mtoto kuzungumza masuala ya uzazi hivyo tumeona ipo haja ya kujadiliana na wadau wengine ili kuuweka sawa,” amesema
Mmoja ya washiriki katika mkutano huo, bi Amina Salum Halfan kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, amesema kupitia muongozo huo pia utasaidia kuepusha mimba umri mdogo ambazo wanazipata kutokana na ukosefu wa Elimu ya afya ya uzazi.