Home LOCAL NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI AKAGUA MRADI WA UPANUZI WA UWANJA...

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI AKAGUA MRADI WA UPANUZI WA UWANJA WA NDEGE SONGEA,AFURAHISHWA NA KAZI ILIYOFANYIKA

 Naibu Waziri wa ujenzi na uchukuzi Atupele Mwakibete wa kwanza kushoto akikagua mnara wa kuongozea ndege alipotembea  mradi wa upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Songea,katikati Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Songea Dkt Frederick Segamwiko.


Naibu waziri wa ujenzi na uchukuzi Atupele Mwakibete kushoto,akitoa maelekezo kwa Meneja wa Tanroads mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ephatar Mlavi kuhusiana na upanuzi wa kiwanja cha ndege Songea ambacho kimefanyiwa upanuzi kwa lengo la kuruhusu ndege kubwa kutoa katika kiwanja hicho.

Naibu Waziri wa ujenzi na uchukuzi Atupele Mwakibete wa kwanza kushoto akitembelea eneo la mradi wa upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Songea,katikati mwakilishi wa mkuu wa wilaya ya Songea Dkt Frederick Segamwiko na kulia meneja wa Tanroads mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ephatar Mlavi.

Meneja wa Tanroads mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ephatar Mlavi kulia akitoa taarifa ya ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege Songea kwa Naibu Waziri wa ujenzi na uchukuzi Atupele Mwakibete.


Naibu Waziri wa ujenzi na uchukuzi Atupele Mwakibete katikati akikagua sehemu ya kuruka na kutua ndege katika kiwanja cha ndege Songea kilichofanyia upanuzi na ukarabati mkubwa kwa gharama ya zaidi ya Sh,bilioni 37.9,kulia Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Songea Dkt Frederick Segamwiko na kushoto Meneja wa Tanroads mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ephatar Mlavi.



Sehemu ya kutua na kurukia ndege katika kiwanja cha ndege Songea mkoani Ruvuma kama inavyoonekana baada ya ukarabti mkubwa uliofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya usimamizi wa wakala wa barabara nchini Tanroads mkoa wa Ruvuma.


Na: Muhidin Amri, Songea

NAIBU Waziri wa ujenzi na uchukuzi Atupele Mwakibete,amekagua mradi wa ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Songea ambacho Serikali imetoa Sh.bilioni 37.09 kutekeleza mradi huo.



Akizungumza mara baada ya kukagua ukarabati huo,Naibu Waziri  Mwakibete amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo ambazo zinakwenda kuufungua mkoa wa Ruvuma na Tanzania kwa ujumla katika usafiri wa anga.

Naibu Waziri Mwakibete ameridhika  na kazi iliyofanywa na wakala wa Barabara nchini(Tanroads)mkoa wa Ruvuma katika utekelezaji wa mradi huo  muhimu kiuchumi.


Hata hivyo,ameiagiza Tanroads kumsimamia mkandarasi kampuni ya Chico ili kukamilisha kazi  zilizobaki ikiwamo kufunga taa  ili kuruhusu  ndege kutua na kuruka saa 24  badala ya kutumika mchana tu.


Naibu Waziri Mwakibete,ameishauri Tanroads na mamlaka ya viwanja vya ndege(TAA)kuangalia namna ya kuongeza ukubwa wa uwanja huo kwa kuanza mchakato wa kuwalipa fidia baadhi ya wananchi wanaoishi maeneo jirani,hasa upande wa Barabara kuu ya Songea-Mbinga ili kuwezesha ndege kubwa zaidi kama AirBus na Dream liner katika kiwanja hicho.



“nawaomba wenzetu wa Tanroads na mamlaka ya viwanja vya ndege nchini,kwa sasa ndege pekee inayoweza kutua katika uwanja huu ambayo ni kubwa zaidi ni aina ya Bombadier tu,lakini ndege kama AirBus au Dreamliner haziwezi kutua,kwa hiyo ni vyema kuanza mchakato wa kuongeza ukubwa wa  kiwanja chetu”alisema.



Mwakibete alieleza kuwa,mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula,uchimbaji wa makaa ya mawe na kuna ziwa maarufu la nyasa ambapo lengo  kubwa la Serikali ya awamu ya sita kiwanja hicho kitatumika kusafirisha bidhaa  ikiwamo makaa ya mawe.


Aidha,amewataka wakazi wa mkoa wa Ruvuma na mikoa jirani ya nyanda za juu kusini,kuhakikisha wanatumia  fursa ya upanuzi wa kiwanja hicho kuongeza uzalishaji wa bidhaa na kusafiri kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kibiashara na utalii.



Alisema,upanuzi na ukarabati wa kiwanja cha ndege Songea kunatoa fursa za uwekezaji na utalii kwa sababu mkoa wa Ruvuma una vivutio vingi na vya kila aina ikiwamo Ziwa Nyasa,Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na maeneo mengi yenye utalii wa kihistoria na kiutamaduni.


Kwa upande wake Meneja wa wakala wa Barabara Tanroads mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ephatar  Mlavi alisema, kazi ya upanuzi na ukarabati wa kiwanja cha ndege Songea ilianza 2019 ulitakiwa kukamilika mwezi Disemba 2020.


Hata hivyo alisema,kutokana na kuongezeka kwa baadhi ya kazi walilazimika kuongeza muda hadi tarehe 30 JUNI 2022 na muda wa matazamio ni miezi kumi na mbili.

Alisema, gharama ya mradi ni Sh.bilioni 37.9 na hadi sasa mkandarasi ameshalipwa shilingi bilioni 21.381 na fedha nyingine ambazo ni Sh.bilioni 2.1 zinaendelea kushughulikiwa ili ziweze kulipwa na kazi  hiyo imefikia asilimia 90.


Alisema,kazi zilizofanyika hadi sasa ni ujenzi wa sehemu ya kutua na kurukia ndege,upanuzi wa sehemu ya usalama wa uwanja kila upande,sehemu ya maegesho ya ndege,kuchora mistari na kujenga mifereji yenye urefu wa mita 6000.


Aidha alitaja kazi nyingine zilizofanywa na mkandarasi ni kujenga uzio kuzunguka uwanja,kujenga barabara mbili ndani  na nje ya uzio kuzunguka uwanja,kufunga taa za kuongozea ndege ambazo ujenzi wake utakamilika mwishoni mwa mwezi Julai ili kuruhusu ndege kuruka na kutua usiku.


Kwa mujibu wa Mlavi kazi nyingine ni zilizofanyika ni ujenzi wa jengo la kuongozea ndege(Control Tower) ambalo umefikia asilimia 75,ununuzi wa gari la zimamoto lenye uwezo wa kubeba maji lita 10,000 ambalo limeshaagizwa,kujenga jengo la kupokea na kusambaza umeme.


Mlavi alisema,mkandrasi kwa sasa anaendelea kukamilisha kazi ndogo ndogo zilizobaki ambazo zitafanywa  katika muda wa matazamio na atakabidhi kazi zote Mwezi Agosti mwaka huu.


Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Songea Dkt Frederick Sagamiko,ameishukuru Serikali kwa kazi nzuri ya upanuzi wa kiwanja cha ndege Songea na kuhaidi kwamba wananchi wa Songea na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla watahakikisha wanatumia kiwanja hicho  kupanua shughuli za kiuchumi ikiwamo kufanya biashara na kusafirisha bidhaa mbalimbali kwenda mikoa mingine na nje ya nchi.


Dkt Sagamiko ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea alisema,katika mkoa wa Ruvuma kuna fursa nyingi ambazo kupitia kiwanja hicho watabadili mtazamo katika shughuli za kilimo kwa kuanza kulima maua na bustani za mboga mboga ambazo mahitaji yake ni makubwa hapa nchini na nje ya nchi.


Kwa upande wake kaimu meneja wa kiwanja cha Ndege Songea Jafari Mbayo alisema,mara baada ya serikali kufanya ukarabati  na upanuzi wa kiwanja hicho idadi ya abiria wanaotumia usafiri wa ndege imeongezeka  hadi kufikia 72.


Alisema, hali hiyo inaonesha kuwa kuna abiria wengi wanaosafiri  kwa kutumia kiwanja cha ndege cha Songea kutokana na ukweli kwamba usafiri wa ndege ni wa haraka na salama.


Previous articleWIZARA YA MADINI YASHUSHA NEEMA KWA WACHIMBAJI WADOGO.
Next articleRC SINGIDA APIGA MARUFUKU WANANCHI KUCHOMA MKAA NDANI YA MSITU WA MGORI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here