(PICHA NA: HUGHES DUGILO)
DAR ES SALAAMÂ
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), imesema kuwa katika Mwaka wa fedha wa 2022-2023 zaidi ya Sampuli 200,000 zilifanyiwa uchunguzi katika maabara za Mamlaka hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Sheria.
Hayo yamebainishwa na Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt Fidelice Mafumiko alipokuwa akiwasilisha mada ya namna Mamlaka hiyo inavyotekeleza majukumu yake katika kikao kazi na Wahariri wa Habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kilichofanyika leo Novemba 30, 2023 Jijini Dar Es Salaam.
Ameeleza kuwa awali katika mwaka wa fedha wa 2021-2022 kumekuwepo na wastani wa sampuli na vielelezo 155.817 sawa na asilimia 139.94Â ya lengo la wastani wa uchunguzi wa sampuli 111.349 uliifanyika.
“Umuhimu wa Huduma za uchunguzi wa kimaabara ni pamoja na kuleta haki, amani na utulivu wa nchi kwa kutoa ushahidi mahakamani kwenye mashauri yanayotokana na uchunguzi wake” ameeleza Dkt.Mafumiko.
Ameongeza kuwa faida nyingine ni pamoja na kutatua migogoro kwenye jamii ikiwa ni pamoja na ushahidi wa wazazi kwa mtoto au mrithi.
Faida nyingine ni kuwezesha upandikizaji wa figo kwa wagonjwa kwa ushirikiano na madaktari Bingwa na kuwezesha kumtambua ubora na usalama wa Bidhaa za viwandani na kilimo kwaajili ya kulinda afya ya jamii.
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Ina Maabara tatu zilizopo chini ya Kurugenzi ya Huduma za Sayansi Jinai zenye jukumu la kuchunguza Sayansi Jinai, Baiolojia na Vinasaba, maabara ya uchunguzi wa Sayansi jinai Toksikolojia, pamoja na maabara ya uchunguzi wa Sayansi jinai Kemia.