Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa kushirikiana na Mtandao wa Wathibiti Ubora wa Elimu ya Juu Barani Afrika (African Quality Assurance Network – AfriQAN), imeaandaa Kongamano la Mtandao wa Wathibiti Ubora wa Elimu ya Juu Barani Afrika litakalofanyika tarehe 28 – 30 Novemba 2023 katika Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam.
Kongamano hili lenye lengo la kujadili mchango wa uthibiti ubora katika kuongeza umahiri wa elimu ya juu Barani Afrika linatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki wapatao 100, wakijimuisha: Taasisi za Uthibiti Ubora wa elimu ya juu; Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu na Wakuu wa Taasisi za Elimu ya Juu; Jumuiya na Asasi za Kimataifa na Kikanda zinazojihusisha na Elimu ya Juu; Wanataaluma; Mabaraza na Bodi za Usajili wa Wataalamu; na Wadau wa Elimu ya Juu kutoka ndani na nje ya nchi.
Mgeni Rasmi tarehe 28 Novemba 2023 katika ufunguzi wa kongamano hili ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Profesa Adolf Mkenda.