Home LOCAL MAJALIWA ATEMA CHECHE MIMBA ZA WATOTO WA SHULE

MAJALIWA ATEMA CHECHE MIMBA ZA WATOTO WA SHULE

*Ahoji ni kwa nini kesi mbili tu ziko mahakamani, awataka RC, Ma-DC wachukue hatua kwa wahusika*

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Francis Michael na Wakuu wa Wilaya zote za mkoa huo wahakikishe wanawasaka watu wote wanaotuhumiwa kuwapa mimba watoto wa kike.

“Tangu Januari hadi sasa, mkoa huu una kesi 59 za wasichana walioacha shule kwa sababu ya ujauzito lakini ni kesi mbili tu zimeeenda mahakamani. Hizo 57 ziko wapi au zimeishia wapi? Ni nani anazuia kesi hizi zisiende? Jeshi la Polisi, ni kwa nini hatuwafikishi watuhumiwa kwenye vyombo vya sheria?, amehoji.

“RC na Ma-DC wote kaeni na Kamati zenu za Ulinzi mbainishe wahusike na mhakikishe hatua kali zinachukuliwa dhidi ya wote waliohusika,” amesema Waziri Mkuu leo (Alhamisi, Novemba 23, 2023) wakati akitoa agizo hilo mara baada ya kukagua ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana Ileje.

Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani humo kwa ziara ya siku tatu, amesema taarifa za mkoa huo siyo kwani kesi hizo 59 ni kwa shule za sekondari na hazijumuishi shule za msingi.

Amewakemea vijana wanaopenda kutembea na watoto wa shule waache tabia hiyo mara moja kwani wanakatisha maisha ya baadaye ya watoto hao. “Sheria iko wazi katika kosa hili. Adhabu yake ni miaka 30, kijana kabla hujamfuata binti jiulize una miaka mingapi, sababu tukikufunga utarudi ukiwa mzee,” amesema.

Akisisitiza haja ya kuwalinda mabinti, Waziri Mkuu amesema: “Hawa ni watoto wetu, tunapaswa tuwalee ili wakue na kuja kushika majukumu ya nchi. Rais Samia amewekeza kwao kwa kutoa elimu bila ada. Tunapaswa tuhakikishe wanatimiza ndoto zao, kwa hiyo tuwalee ili waweze kuhitimu,” amesisitiza.

Amewaomba masheikh na wachungaji wakemee tabia hiyo kupitia mahubiri ya kwenye ibada.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewapongeza wana-Ileje kwa kujenga maabara ya kompyuta kwenye shule hiyo yenye mikondo ya kidato cha kwanza hadi cha nne ili kuhimiza matumizi ya TEHAMA.

“Nimefurahi kuona mna jengo maalumu la TEHAMA. Hii inaakisi malengo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutaka TEHAMA isambae nchi nzima.”

Amesema amefurahi pia kusikia Halmashauri hiyo ina lengo la kuifanya shule hiyo iwe na kidato cha tano na sita. “Mkurugenzi Mtendaji fanyeni maamuzi ili madarasa ya kidato cha tano na sita yajengwe na muweze kuwapa fursa watoto wa kike wa wilaya hii. Pia mtatoa chachu kwa hawa wa kidato cha kwanza hadi nne ili wasome kwa bidii,” alisema.

Previous articleREA: VIJIJI VYOTE KUFIKIWA NA UMEME IFIKAPO MWEZI JUNI,2024
Next articleKONGAMANO LA WATHIBITI UBORA WA ELIMU BARANI AFRIKA KUFANYIKA JIJINI DAR
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here