Wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika Kijiji cha Nyambogo Kata ya Nyakafulu Wilayani Mbogwe Mkoani Geita Wamelalamikia hali ya ucheleweshwaji wa mgao wa mifuko inayosadikiwa kuwa na dhahabu jambo linalopelekea kukosa fedha.
Wachimbaji hao wametoa lawama zao mbele ya Waziri wa madini katika mkutano uliofanyika Septemba 3 katika mgodi huo uliolenga kutatua kero za wachimbaji, ambapo walizitupia lawama ofisi za madini za mkoa mpya wa kimadini Mbogwe na kusema kuwa maofisa madini wamekua wakichelewesha mgao.
Akijibu hoja hiyo Waziri mwenye dhamana ya madini nchini Doto Biteko, amewaeleza wachimbaji hao kuwa kucheleweshwa kwa mgao katika machimbo hayo kunatokana na ofisi za madini katika Mkoa mpya wa kimadini Mbogwe kuzidiwa na majukumu kwani wanahudumia pia katika machimbo mengine yaliopo katika Wilaya ya Bukombe pamoja na halmashauri ya Nyang’wale.
Waziri Biteko aliwataka watumishi wa madini wa Mkoa wa Madini Mbogwe kugawa mifuko ya mawe yanayosadikiwa kuwa na dhahabu kwa siku nne mfululizo ili kupunguza msongamaono huo.