DODOMA.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Benki ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Ujerumani (KfW) Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika Bw. Christoph Tiskens aliyeambatana na viongozi waandamizi wengine kutoka katika Shirika hilo na Serikali ya Ujerumani.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo katika ofisi za Wizara jijini Dodoma, Prof Makubi kwa niaba ya Serikali ameishukuru Serikali ya Ujerumani kuendelea kudumisha mahusiano na ushirikiano yanayowezesha uboreshaji wa Sekta mbalimbali nchini ikiwemo afya.
Prof. Makubi amesema Ujerumani imeendelea kuchangia mfuko wa afya wa Pamoja (Health Basket Fund) toka mwaka 2013 ambapo kupitia shirika la KfW limejenga na kuboresha miundombinu ya afya katika mikoa ya Tanga na Mtwara.
Aidha, Prof. Makubi amesema ushirikiano wa sasa umelenga katika upande wa TEHAMA utasaidia mfumo wa mpango wa Bima ya afya kwa wote ambapo Euro milioni 7 zimetengwa katika kipindi cha miaka minne kuisaidia Shirika la Bima ya Afya (NHIF) ili kutimiza lengo hilo.
Prof. Makubi amesema katika kuboresha huduma za UKIMWI na uzazi kwa akinamama masikini kupitia mradi wa Tumaini la mama umeweza kuwafikia kinamama Zaidi ya milioni 1.1 ambao wamenufaika kwa kupata huduma bora kupitia bima za NHIF na CHF katika baadhi ya mikoa nchini.
Kuhusu wimbi la tatu la Corona Prof. Makubi amesema asilimia 40 ya wagonjwa waliolazwa katika Hospitali za mikoa mbalimbali walikua wanahitaji hewa ya Oksijeni hivyo kufanya Serikali kutekeleza miongozo iliyotolewa na Shirika la afya Duniani (WHO) ili kukabiliana na wimbi hilo.Naye Mkurugenzi Christoph Tiskens ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Ujerumani kupitia Mashirika yake katika kuboresha sekta mbalimbali nchini ikiwemo ya afya na kutaka ushirikiano huo uweze kuwa chachu ya huduma bora za afya kwa wananchi na kupunguza umasikini.