Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akisikiliza hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mhe. Abdel Fatah Al -Sisi, aliyoifanya kwa njia ya mtandao wakati wa Kongamano la Kimataifa la Ushirikiano la Misri lililofanyika Cairo nchini Misri.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akiteta jambo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Ushirikiano na Mahusiano ya Kimataifa wa Namibia, Mhe. Netumbo Nandi- Ndaitwah baada ya Kongamano la Kimataifa la Ushirikiano la Misri lililofanyika Cairo nchini Misri.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, akifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa wakati wa Kongamano la Kimataifa la Ushirikiano la Misri lililofanyika Cairo nchini Misri.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango – Misri)
Na. Josephine Majula, WFM, Cairo- Misri
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amewakaribisha Wawekezaji kutoka Jamhuri ya Kiarabu ya Misri kuwekeza na kufanya biashara na Tanzania kutokana na uwepo wa mazingira rafiki na fursa za uwekezaji.
Waziri nchemba ametoa rai hiyo mjini Cairo Misri, wakati wa Kongamano la Kimataifa la Ushirikiano la Misri (Egypt International Cooperation Forum) lililowakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo washirika wa maendeleo kutoka Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Ulaya, Jumuiya ya Ushirikiano wa Uchumi na Maendeleo, Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia.
Dkt. Mwigulu alisema kuwa kuna umuhimu wa kusisitiza kukuza mahusiano ya kimataifa hususan kwa nchi za kiafrika zinazoendelea na kuweka mikakati endelevu ya kupambana na athari za janga la Uviko – 19, ili kukuza uchumi.
“Katika Kongamano hili tumejadilia namna bora ya kusaidiana katika mitaji hususan katika nchi zenye Taasisi za Kifedha zenye uwezo wakutoa fedha katika mazingira ya Uviko- 19 kutokana kuathiri shughuli nyingi za kiuchumi”, alieleza Dkt. Nchemba.
Aidha Dkt. Nchemba ameipongeza Wizara ya Ushirikiano ya Kimataifa ya Jamhuri ya Kiarabu ya Misri kwa kuandaa kongamano hilo kwa kuwa limeunganisha wadau kutoka sehemu mbalimbali duniani na kutoa fursa ya kuweza kujadiliana na kupeana uzoefu kwa lengo la kuleta maendeleo.
Vilevile ameahidi kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Kiarabu ya Misri katika nyanja mbalimbali ikiwemo masuala ya uchumi, uwekezaji na biashara ili kukuza uchumi kati ya nchi hizo.
Kongamano la Kimataifa la Ushirikiano la Misri (Egypt International Cooperation Forum) linalofanyika kwa siku 2 limehudhuriwa na nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, Malawi, Senegal, Kenya, Namibia na Zambia.