Home LOCAL DHANA YA MAGEUZI NI UWANJA MPANA – OTHMAN

DHANA YA MAGEUZI NI UWANJA MPANA – OTHMAN

Na: Halfan Abdulkadir

Makamu Mwenyekiti wa ATC-Wazalendo Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman amesema dhana ya mageuzi ni uwanja mpana, ambapo utekelezaji wake ni kutoka mbali, kuanzia Chaguzi za haki na demokrasia ndani ya Chama.

Mheshimiwa Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo leo katika Mkutano Maalum wa Viongozi Wapya wa Chama hicho, kutoka Mikoa ya Wete na Micheweni kichama, huko katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Bopwe-Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Amesema kuwa Chama hicho ni taasisi inayosimamia harakati za kuleta mageuzi ya kisiasa na ili hatimaye kuongoza Nchi, hivyo ni wajibu wa kila kiongozi kuanza na mabadiliko ya nafsi yake, kwa kuzingatia misingi ya uadilifu, haki, kuvumiliana, umoja na mashirikiano mbele ya wananchi wote.

Akiongelea kuhusu nafasi ya vijana katika harakati za siasa na kupigania maendeleo na Mamlaka ya Nchi, Mheshimiwa Othman amewakumbusha viongozi kuelewa kwamba mageuzi ya kweli yanayojali maisha ya wananchi, hayatofikiwa kwa kuendelea kuighilibu sehemu hiyo muhimu ya jamii, kwa seti ya jezi za Mpira.

Hivyo amesema kushindwa kuelewa kwa viongozi na watu waliopewa nafasi mbalimbali, kwamba mamlaka ni amana na dhamana, ndiko kunakoendelea kupelekea hali duni na kudhoofika kwa hali ya maisha ndani ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla.

Aidha amesema, “ieleweke kwamba haya siyo ya kisiasa bali ni kutokana na ukweli kwamba maisha ya watu ndani ya Nchi hii yanakoelekea hayaleti matumaini kutokana na ukosefu wa kujipanga, kushindwa kuzingatia haki na uadilifu, na pia kukosekana kwa hisia za kujali dhamana na maadili ya uongozi”.

“Naomba niwakumbushe kwamba Nafasi tulizopewa na Wenzetu ni amana na ni dhamana, hivyo kuzitendea haki ni wajibu, kwani hilo ni jambo la watu ambalo kwamujibu wa mafunzo ya Wazee wetu, jambo la watu halipaswi kulifanyia khiyana, na kufanya khiyana madhara yake ni makubwa hata kwa Vizazi vijavyo”, ameasa Mheshimiwa Othman.

Amefahamisha kuwa Zoezi la kuwapata Viongozi hao Wapya, kupitia Uchaguzi wa Ndani wa Chama hicho wa hivi karibuni ni katika Mitihani iliyopita salama, na hivyo ili kuepusha hisia za kurudi nyuma katika kuendeleza siasa, ni vyema kwa wote waliojitokeza kugombea waamini juu ya hali ya matokeo katika ushindani wowote, chini ya Kaulimbiu isemayo, “tuchague mmoja tubaki wamoja”.

Mheshimiwa Othman amechukua fursa hiyo kuwapongeza Wanachama waliojitokeza kugombea Nafasi mbalimbali za Uongozi wa Chama hicho, kupitia Mchakato wa Uchaguzi wa Ndani ya chama wa hivi karibuni, na kusisitiza kwa kusema, “napenda niwapongeze zaidi wale Wagombea ambao walijitokeza, wakashindwa na wakakubali kushindwa”.

Naye, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Bw. Salim Bimani, amewakumbusha Viongozi wapya wa kutambua kwamba dhamira ya msingi ya Chama hicho siyo kupata nafasi za Ubunge, Uwakilishi wala Udiwani, bali la muhimu Zaidi ni kuzingatia umoja na utumishi wa haki, maadili na uadilifu kwa Wazanzibari wote.

Mratib wa ACT-Wazalendo kisiwani Pemba, Bw. Said Ali Mbarouk amepongeza juhudi za Wapenzi na Wafuasi wa Chama hicho, kuendeleza msimamo wa kuungamkono juhudi za kisiasa, licha ya mazingira magumu yanayowakabili, akisema hiyo inabaki kuwa ni dhima na deni kwa Viongozi wa sasa na baadae.

Kwa upande wake, Katibu wa Chaguzi wa ACT-Wazalendo, Bw. Muhene Said Rashid amesema Zoezi la kuwapata Viongozi wa Ngazi zote wa Chama hicho, kuanzia Matawi yote takriban 678 na Majimbo 50 ya Unguja na Pemba, lililoanza mwezi wa Agosti, Mwaka huu, limeendelea vyema na kufikia asilimia 93.8, sambamba na utaratibu wa kumpata Mgombea atakayepeperusha bendera ya Chama hicho katika Uchaguzi Mdogo wa Uwakilishi wa Jimbo la Mtambwe, unaotarajiwa kufanyika mnamo Oktoba 28, 2023. kufuatia kifo cha aliyekuwa Muwakilishi wake, Marehemu Habib Ali Mohamed.

Mkutano huo maalum ulioanza kwa Dua iliyosomwa na Sheikh Khatib Omar Salim sambamba na Burudani mbalimbali za Kisiwani hapa, umelenga katika Kuwakusanya baadhi ya Watendaji Wakuu wa wakiwemo Wenyekiti, Wabunge, Wajumbe wa Kamati Kuu, pamoja na Kuwahutubia Viongozi Wapya wa Mikoa ya Wete na Micheweni kichama, katika Mkoa wa Kaskazini Pemba, waliopatikana kupitia Mchakato wa hivi karibuni wa Uchaguzi, ndani ya Chama hicho.

Othman ambaye ameambatana na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib, yupo Kisiwani Pemba, kwa Ziara Maalum ya Siku 4 kwaajili ya Shughuli za Chama na Serikali, tangu aliopowasili mapema September 15 na kupokelewa na Viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama.

Previous articleSEKTA YA MADINI KUFUNGAMANISHWA NA SEKTA NYINGINE ZA KIUCHUMI
Next articleRAIS DKT. SAMIA AZUNGUMZA NA WANANCHI LIWALE MKOANI LINDI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here