Serikali ya Tanzania imebaini kuwa ugonjwa unaoua watu kusini mwa Tanzania ni homa ya Mgunda.
Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu amewaambia waandishi wa habari kuwa upimaji wa sampuli za wagonjwa waliokuwa wakiugua katika Wilaya ya Ruangwa katika Mkoa wa Lindi umethibitisha mlipuko huu kuwa wa ugonjwa unaoitwa kitalaamu Leptospirosis, Field Fever au kwa lugha ya Kiswahili inajulikana kama Homa ya Mgunda.
Waziri Ummy amesema hayo leo mara baada ya kutembelea Wilaya ya Ruangwa katika Mkoa wa Lindi ambako kumezuka Mlipuko wa Ugonjwa huo na kuzungumza na Waandishi wa Habari.
Kwa mujibu wa Waziri Ummy Homa ya Mgunda ni miongoni mwa magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na unasababishwa na Bakteria aina ya Leptospira interrogans.