NA: MWANDISHI WETU DODOMA
KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amewataka wakandarasi kuzingatia ubora katika ujenzi wa majengo ya Ofisi za Serikali katika eneo la Mtumba na kukamilisha kwa wakati.
Ametoa kauli hiyo alipokagua maendeleo ya Ujenzi wa Majengo ya Ofisi za Serikali unaoendelea eneo la Mtumba Jijini Dodoma ambapo amekagua baadhi ya majengo ikiwemo la Ofisi yake, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Maji na Wizara ya Fedha.
Dkt. Yonazi amehizima kwa kila mkandarasi kuhakikisha anazingatia ubora na viwango vinavyotakiwa huku wakizingatia thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali.
“Dhamira ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuona majengo haya yanakamilika kwa wakati na yawe na viwango vinavyotakiwa, bila kuwa na delays zozote ili kuhakikisha watumishi wote wanahamia haraka na kuendelea na utekelezaji wa majukumu yao na kuliletea Taifa maendeleo yanayotakiwa,” alisema Dkt. Yonazi
Awali alipongeza kwa hatua iliyofikiwa ya ujenzi huo na kueleza kuwa, Serikali imejipanga kuhakikisha hakuna mkandarasi atakayekwama kwa sababu zozote zile.
“Serikali imedhamiria kuona hakuna mikwamo katika ujenzi huu, hivyo msirudishe nyuma jitihada hizo, hakikisheni mnamaliza mradi huu kama ilivyoelekezwa,” Alisisitiza Dkt. Yonazi