Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Geita(GEDIFA) Mnenge Suluja akizungumza baada ya Mbunge Kanyasu Kugawa vifaa vya Michezo. |
Na.:Costantine James, Geita.
Katika hali ya kuibua, kuendeleza na kukuza vipaji kwa vijana mbalimbali mkoani Geita mbunge wa jimbo la Geita mjini Mhe, Constantine Kanyasu ameunga mkono juhudi za kukuza vipaji kwa vijana kwa kudhamini michuano ya ligi daraja la nne inayofanyika katika wilaya ya Geita mkoani Geita.
Mhe, Kanyasu ametoa udhamini katika ligi daraja la nne ngazi ya wilaya kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo kwa kutoa milioni 10 kila mwaka kwa kipindi cha misimu mitatu mfululizo ndani ya wilaya ya Geita.
Kanyasu amesema ameamua kudhamini michuano hiyo kutokana na ligi za wilaya kutokuwa na wadhamini hali ambayo ilikuwa inapelekea mashindano hayo kuendeshwa kwa ukata mkubwa wa pesa.
Amesema katika kipindi cha miaka mitatu akiwa kama mdhamini wa michuano ya Gediva district Kanyasu cup atatoa vifaa vya michezo ikiwemo jezi, mipira, pamoja na matibabu kwa wachezaji wanao pata majeraha pindi wakiwa viwanjani na atahakikisha analipa posho za waamuzi wananosimamia michuano hiyo.
Kanyasu amesema miaka yote alikuwa ananunua vifaa vya michezo nakugawa kwenye vilabu mbalimbali lakini ameamua kubadilisha na kudhamini michuano hiyo kwa lengo la kuibua vipaji zaidi kwa vijana ili waweze kucheza kwenye vilabu vikubwa hapa nchini hata nje ya nchi.
Kwa upande wake katibu wa chama cha mpira wa miguu wilaya ya Geita (GEDIFA) Mnenge Suluja amemshukuru Mbunge wa jimbo la Geita Mjini Mhe, Constantine Kanyasu kwa kudhamini mashindano hayo kwa misimu mitatu mfululizo.
Suluja amesema mashindano hayo yanahusisha vijana zaidi ya 210 kutoka katika wilaya ya Geita ambapo timu mbili zitakazo maliza mshindi wa kwanza na wapili watapata nafasi ya kupanda kwenda kucheza ligi ya mkoa.
Amesema udhamini wa mbunge Kanyasu kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo wao kama chama cha mpira wa miguu wilaya ya Geita (GEDIFA) umewapunguzia gharama za uendeshaji wa michuano hiyo pamoja na kuwarahisishia timu kupata vifaa vya michezo.
Nao baadhi ya wawakilishi wa timu zinazoshiriki michuano hiyo wamemushukuru mbunge wa jimbo la Geita vijini mhe, Constantine Kanyansu kwa kudhamini michuano hiyo pamoja na kutoa vifaa vya michezo kwani itawawezesha kushiriki kwa urahisi katika michuano hiyo.
Wamesema walikuwa wanapata changamoto ya kujichagisha kwa lengo la kuendesha timu zao ikiwemo kununua vifaa vya michezo hali iliyokuwa inawafanya washindwe kucheza vizuri lakini sasa udhamini wa mhe Mbunge Kanyasu umemaliza changamoto zote walizokuwa wanazipata hapo awali.
Naye kapteni Richard Nzagamba mdau soka kutoka mkoani Geita amempongeza Mhe, Constantine Kanyasu amesema udhamini huo utasaidia kuibua na kuendeleza vipaji vya soka kwa vijana ndani ya mkoa wa Geita.