Manispaa ya Tabora imeanza rasmi leo Agosti 28,2023 kutumia mfumo wa E-MIKUTANO katika vikao vyake ili kuwapa fursa wajumbe wa vikao hivyo kushiriki kikamilifu hata kama wapo nje na Manispaa.
Katika kikao cha Morning Session cha leo, wajumbe kadhaa waliweza kushiriki kwa mfumo wa mawasiliano ya njia ya video ( Vedeo Conferencing) akiwamo Ndugu Pius Haule (Mkaguzi wa Ndani), Ndugu Robert Matungwa ( Mwanasheria ), Ndugu Nelson Mwankina( Mchumi), Injinia Asteria Shija ( Mhandisi wa Manispaa) pamoja na Ndugu Syliverster Mhumpa ambae ni Afisa Ugavi wa Manispaa.
Malengo mahsusi ya mfumo wa E-MIKUTANO ni kuwezesha watumishi na Viongozi wa Serikali kuhudhuria vikao vya msingi na vya kisheria bila kuwa na kizuizi cha umbali walipo.
Hivyo Manispaa ya Tabora kuanza kutumia mfumo huu katika vikao vyake kwanza ni kuleta tija kwenye vikao husika kwani wajumbe watatoa mawazo, ushauri na maoni yao badala ya wawakilishi wao ambao wangehudhuri vikao hivyo na ukizingatia wawakilishi siku zote hawana maamuzi na hata ushauri wao huwa haupewi uzito sana ukilinganisha na wajumbe husika.
Sambamba na mfumo huu, vilevile Manispaa ya Tabora imeshaachana na matumizi ya Kablasha kwenye vikao vyake, hii ikiwa inachagizwa na matumizi ya Vishikwambi pamoja na Mfumo wa TEHAMA wa uendeshaji wa vikao vya Serikali (E-BOARD).
Hivyo Manispaa ya Tabora imeweza kununua Vishikwambi kwa idadi ya Wakuu wa Sehemu, Vitengo pamoja na Waheshimiwa Madiwani.
Kwa ujumla wake sasa, ukiunganisha uwepo wa Vishikwambi ambavyo ni vya kisasa kabisa, uwepo wa mfumo wa E-BOARD unaowesha upatikanaji wa taarifa na nyaraka muhimu mtandaoni , pamoja na mfumo wa E-MIKUTANO ambao unawesha mtumishi ama kiongozi kuhudhuria kikao kwa mawasiliano ya njia ya video, basi vyote hivi vinaifanya Manispaa ya Tabora kutokuwa mstari wa nyuma katika matumizi ya teknolojia ya mtandao.
Matumizi haya ya Teknolojia ya Mtandao kwaujumla wake yanaongeza tija sana katika utekelezaji wa dira ya Halmashauri pamoja na maelekezo mahsusi ya Serikali kwani Mtumishi ama kiongozi anafanya kazi zake na kuhudhuria vikao muhimu vya maamuzi akiwa popote pale.