Baadhi ya wanawake walioshiriki semina ya Kupinga Ukatili, Rushwa ya Ngono kwa Wanawake wakiwa katika picha pamoja mara baada ya semina hiyo.
Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM.
Katika kuhakikisha wanawake wanashirki kwenye ngazi mbaalimbali za uongozi na kuwa na wigo mpana wa kushiriki katika harakati za kugombea nyadhifa hizo, bado kundi hilo muhimu limeonekana kukutana na changamoto mbalimbali zinazowafanya kukata tamaa na wengine kuachana kabisa na masuala ya uongozi.
Hata hivyo kuna jitahada kubwa zinazofanywa na wadau mbalimbali wakiwemo wanaharakati wa haki za Binaadamu, makundi ya wasomi na jamii nzima kwa ujumla kuhakikisha wanawake wanashiriki kwenye masuala ya uongozi huku wengine wakijitosa moja kwa moja kwenye siasa na kugombea nafasi mbalimbali katika vyama vya siasa na ngazi za Serikali.
Sauti ya Jamii Kipunguni ni Kikundi cha Kijamii kinachopamabana kuinua haki za wanawake na wasichana ikiwa ni pamoja na kupinga rushwa ya ngono, ukeketaji, pamoja na kuinua wanawake kiuchumi.
Aidha Sauti ya Jamii Kipunguni inatekeleza Kampeni ya kuwezesha uelewa wa haki kuzuia rushwa ya ngono ndani ya jamii.
Kikundi hiki kimekuwa msaada mkubwa sana kwa wanawake na wasichana wanaotia nia ya kutaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ambapo kimeweza kutoa mafunzo ya madhara ya rushwa ya ngono na uelewa wa haki kwa wanawake na wasichana wenye ndoto ya kuwa viongozi.
Bi. Sea Tumba Khazad ni mkazi wa Kivule kata ya Majohe Jijini Dar es salaam anasema kuwa rushwa ya ngono kwa wanawake na wasichana imekuwa kikwazo sana cha kufikia malengo yao katika kugombea nafasi za uongozi.
“Changamoto hii ya rushwa ya ngono ni kubwa sana kwenye jamii yetu unakuta mtu anakwambia bila mimi kukupitisha huwezi kufanikiwa hivyo ukinikubali tu basi kila kitu chako kitakwenda sawa” anasemaBi Sea ambae ameshawahi kuwa mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa kwa kipindi cha miaka mitano.
Anaongeza kuwa Mradi huo wa unaotekelezwa na kikindi cha Sauti ya Jamii Kipunguni umewezesha kuwaamsha Wanawake na wasichana katika kuelewa haki zao na hatua za kuchukua pale wanapokutana na changamoto ya kuombwa rushwa ya ngono.
“Kwakweli tunamshukuru sana Bwana Bishagazi na kwa kutuletea semina hii kwani nimekuwa ni mkombozi mkubwa wa fikra na kutufanya tuweze kujitambua” Ameongeza Sea.
Mariam Ngomaitala ni mnufaika wa mafunzo yao anasema kuwa semina hiyo imemfumbua macho kumuwezesha kutambua madhara yatokanayo na Rushwa ya Ngono na kwamba anaenda kuwa balozi mwema kwa jamii wa elimu aliyopata kupitia semina hiyo.
Kwaupande wake Salome Masale amesema kuwa moja ya faida aliyopata kupitia semina hiyo ni kujitambua, na kwamba alipitia magumu mengi katika Uchaguzi Mkuu uliopita ikiwemo kuombwa Rushwa ya Ngono na alipokataa, akajikuta akinyimwa nafasi.
“Kupitia semina hii, nimejifunza namna ya kukabiliana, kuviripoti ama kuviepuka vitendo vya Rushwa ya Ngono. Naamini nikiingia katika uchaguzi ujao, nitakuwa imara kuvishinda na kupata mafanikio bila kuruhusu kuathiriwa na vitendo hivyo,” amesema Salome.
Mradi huo wa miezi Mitatu ya wezesha Uelewa wa Haki, Zuia Rushwa ya Ngono Ndani ya Jamii. Umetekelezwa kwa kutoa mafunzo hayo maalum kwa wanawake na wasichana na kuweza kuwajengea uelewa wa namna ya kuweza kudai haki zao pale wanapotakiwa kutoa rushwa ya ngono.
Picha mbalimbali za Mafunzo na Semina ikiendelea.