Naibu waziri wa wizara ya Afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Dkt Godwin Mollel amesema kuwa billion 495 ambazo Rais mama Samia Hassan Suluhu ameipa wizara hiyo zitatumika kufanya mambo ambayo hayakufanyika tangu kupatikana kwa uhuru lakini kwa muda mfupi ambao Rais huyo ameongoza nchi yamewezekana.
Dkt Mollel aliyasema hayo wakati akiongea na waandishi wa habari mkoani Arusha ambapo alisema kuwa fedha hizo zimeelekezwa kwenye masuala yanayogusa maisha ya watu moja kwa moja ikiwemo kuboresha huduma za dharura katika hosipitali nneza taifa, nne za kanda, 22 za rufaaza mikoa na 83 za wilaya.
Alisema kuwa fedha hizo pia zitatumika kununua maghari ya kubebea wagonjwa 423, ujenzi na vyumba vya wagonjwa mahututi(ICU), ununuzi wa vifaa katita hosipitali ya taifa ya Muhimbili,hosipitali maalum tatu, hosipitali za kanda tano,za mikoa 28 na wilaya 29.
Alieleza kuwa pia wataimarisha hewa tiba ya Oksijeni kwa kusimika mitambo 40, manunuzi ya mitungi,vifaa wezeshi na mfumo uatakaowezesha usambazaji wa hewa tiba kwa wagonjwa ambapo pia alisema watanunua CT Scan 30 na kuziweka katika hosipitali zote za mikoa.
“kwanzia Uhuru ni hosipitali mbili tuu za mikoa zenye CT Scan na maeneo mengi walikuwa wakitumia fedha nyingi kusafirisha wagonjwa kwenda kupata huduma hii ambapo ndani ya miezi sita hosipitali zote za mkoa zitakuwa na huduma hiyo ili kuokoa fedha ambazo zinaweza kufanya Mambo mengine ya maendeleo lakini pia kusogeza huduma karibu na wananchi,”Alisema Dkt Mollel.
Alifafanua kuwa watafanya ununuzi wa vitendanishi 10 vya upimaji wa virusi vya UVIKO-19na saratani ambapo kulikuwa na sehemu nne kwaajili ya huduma hiyo na kwasasa zitakuwa 14 pamoja na kununua mashine za X-ray 85 ambazo zitasambazwa kwenye hosipitali zote za taifa,kanda, mikoa na wilaya.