Na: Mwandishi Wetu.
MKUU wa Wilaya ya Temeke kupitia mwakilishi wake Kaimu Ofisa Tarafa Mbagala Theodora Malata ametembelea soko la Makangarawe na kutimiza ahadi ya kuchangia biashara ya kila mfanyabiashara ndogo ndogo sokoni hapo kama pongezi kwa mwitikio wa kuhamia sokoni na kutii agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Katika tukio hiloTheodora alifanya manunuzi kwa wafanyabiashara hao na kutumia kiasi cha shilingi milioni 1.5 kwa kununua bidhaa katika kila meza ya mfanyabiashara mmoja mmoja, na kuwakumbusha wafanyabiashara hao kuwa kupitia mkuu wa wilaya ya Temeke serikali inaonesha kuendelea kutimiza ahadi zake na kueleza umuhimu wa kuhamia sokoni. Alisema Bi. Theodora
“Mheshimiwa DC Jokate amenituma hapa kutimiza ahadi yake,naamini mmeona na mmefurahi wenyewe, tumepita kila meza na kufanya manunuzi kama alivyoahidi, hii ni kwasababu mmeonesha mwitikio mkubwa wa kuhamia sokoni, mahali rasmi ambapo viongozi wetu wameainisha tutumie kufanya biashara.
“Ninyi mmeonesha mwitikio mkubwa na hakuna nguvu iliyotumika kuwahamisha, niwakumbushe serikali yenu inawapenda sana na iko nanyi wakati wote nawasihi waliopo barabarani waendelee kusogea katika maeneo rasmi na masoko yetu yaliyoainishwa,” amesemaTheodora.
“Kwa kweli tumefurahi sana, na tumefurahishwa zaidi na uamuzi wa kununua bidhaa zetu badala ya kutoa kiasi cha pesa kwa kila mmoja wetu, ameonesha kutujali,” amesema mmoja wa wafanyabiashara sokoni hapo.
Soko la Makangarawe ni moja kati ya masoko yaliyopokea mwitikio mkubwa kwa kupokea wafanyabiashara ndogo ndogo (wamachinga) wengi kutoka maeneo yasiyo rasmi na kuwagawia maeneo katika soko hilo.
Mwisho.