Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, Mhe. Abdelmadjid Tebboune amekutana Kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax (Mb.) alipomtembelea Ikulu Jijini Algiers, Algeria tarehe 1 Agosti 2023.
Mazungumzo hayo yamefanyika pembezoni mwa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Algeria ulioanza tarehe 30 Julai 2023 hadi 1 Agosti 2023.
Mazungumzo ya viongozi hao yalijikita katika kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kirafiki na kidiplomasia ili kuweza kutekeleza diplomasia ya uchumi kwa maslahi mapana ya nchi zao.
Aidha, katika kuendelea kuimarisha ushirikiano Waziri Tax pamoja na majukumu mengine, atafanya ufunguzi rasmi wa Ofisi ya Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 2 Agosti 2023 Jijini Algiers.
Ufunguzi rasmi wa ofisi za ubalozi huo ni hatua muhimu hasa wakati huu ambapo viongozi hao wamekubaliana kuinua sekta za uchumi ambazo ni pamoja na biashara.