Na: Mwandishi wetu, DODOMA.
Imeelezwa kuwa Mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 6.7 Mwaka 2020 na kufikia asilimia 7.7 Mwaka 2021 lengo likiwa ni kufikia asilimia 10 ifikapo Mwaka 2025.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini Doto Biteko wakati akiwasilisha mada kwenye Mkutano wa Wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) 2021 katika kujadili Mchango wa Azaki katika Maendeleo ya Nchi uliofanyika katika ukumbi wa Royal Village uliopo jijini Dodoma.
Waziri Biteko amesema mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa umeimarika na kufikia asilimia 7.7 Mwaka 2021 suala ambalo limechangiwa na usimamizi thabiti wa shughuli za madini nchini.
“Mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa ulikuwa asilimia 3.4 mwaka 2015, asilimia 5.2 mwaka 2019, asilimia 6.7 mwaka 2020 na sasa umeongezeka mpaka kufikia asilimia 7.7, tunaamini ifikapo 2025 mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa utakuwa umekafikia asilimia 10,” amesema Waziri Biteko.
Aidha, Waziri Biteko amesema, Mabadiliko ya Sheria ya Madini sura Namba 123 ya Mwaka 2017 yamesaidia kwa kiwango kikubwa kuwafanya watanzania kushiriki katika uchumi wa madini ambapo katika kipindi cha Mwaka 2020/2021 jumla ya kampuni za watoa huduma migodini 961 sawa na asilimia 66 zilikuwa ni za kitanzania na idadi ya kampuni za kigeni zilikuwa 506 sawa na asilimia 34.
Waziri Biteko amesema, uwepo wa idadi kubwa ya watoa huduma wa kitanzania umechochewa kwa kiasi kikubwa na usimamizi wa Sheria ya Madini na Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (Local Content).
Pia, waliziri Biteko amesema Wizara yake imekuwa ikisisitiza wamiliki wa leseni za madini kutoa kipaumbele kwa bidhaa au huduma zinazotolewa na watanzania na kuhakikisha kuwa bidhaa au huduma pekee zinazotolewa na kampuni za kigeni ni zile ambazo hazipatikani nchini.
Sambamba na hilo, Waziri Biteko amesema baada ya uhuru watanzania walikuwa na kiu ya kuona rasilimali madini zinawanufaisha, ndiyo maana aliyekuwa Rais wa Awamu ya Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema, madini tusichimbwe mpaka tutakapo pata wataalamu wazawa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati Stephan Byabato amesema, Wizara ya Nishati inatekeleza Sheria ya Local Content ambapo mpaka sasa wameshatembelea maeneo yote litakalopita bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima Uganda mpaka Chongoleani Tanga ili kubaini mahitaji watakayoweza kuyapata katika maeneo husika, yote hayo ni kwa ajili ya kutimiza Sheria ya Ushirikishwaji wa Wazawa (Local Content).
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la HakiRasilimali – Mtandao wa Asasi za Kiraia unaofanyakazi za kimkakati katika Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi, Rachel Chagoja ameipongeza Serikali kwa kushirikiana na Asasi za Kiraia ambazo zinafanyakazi kubwa ya kuibua changamoto mbalimbali katika jamii nakwamba Shirika lao limekuwa likipata ushirikiano mkubwa kutoka Serikalini kwa kuzifanyiakazi taarifa na tafiti mbalimbali zinazotolewa na shirika lao.
Ameongeza kuwa mkutano huo umewakutanisha wadau sekta za Madini, Gesi, na Mafuta kuweza kupata taarifa mbalimbali za kimkakati kutoka Serikalini ambapo Mawaziri wenye dhmana kwenye Sekta hizo wameweza kuzungumzia mafanikio yaliyopatikana hususani kwenye miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali.