Home LOCAL DKT. MPANGO ATOA WITO NCHI ZA AFRIKA KUWEKEZA KATIKA ELIMU NA AFYA

DKT. MPANGO ATOA WITO NCHI ZA AFRIKA KUWEKEZA KATIKA ELIMU NA AFYA

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa nchi za Afrika kuwekeza katika utoaji wa elimu bora na kutoa huduma bora za afya kwa wananchi ili kuwa na rasilimali watu wenye nguvu watakaoweza kuzalisha kwa tija.

Ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua Mkutano wa siku mbili wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Mtaji Rasilimali Watu unaofanyika kuanzia Julai 25-26, 2023 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (JNICC).

Mhe. Dkt. Mpango amesema inakadiriwa kuwa, katika nchi za kipato cha chini na cha kati, karibu asilimia 40 ya watu wenye umri wa miaka 0 hadi 14 wanaohudhuria shule watakuwa wanatoka Afrika ifikapo mwaka 2050. Aidha, umaskini wa kujifunza utaongezeka kwa asilimia 10 hadi zaidi ya asilimia 60 katika nchi zinazoendelea duniani kote na kutoka asilimia 83 hadi zaidi ya asilimia 90 katika nchi masikini.

“Kutokana na takwimu hizo, Afrika inahitaji kuchukua hatua za haraka kushughulikia idadi ya watu kwa kufanya uwekezaji mzuri katika afya ya watu wetu na elimu ya hali ya juu ambayo itawapa vijana wetu ujuzi unaohitajika kwa mafanikio ya kiuchumi ya nchi zetu”, amebainisha Dkt. Mpango.

Aidha, ameongeza kuwa, Kauli mbiu ya Mkutano huo ya “Kuharakisha Ukuaji wa Uchumi wa Afrika: Kuongeza Uzalishaji wa Vijana kwa Kuboresha Kujifunza, Ujuzi na Uzalishaji wa Vijana” inakumbusha uwezo wa vijana kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika nchi mbalimbali ikiwa nchi zitawekeza kwa uangalifu katika elimu, ujuzi na matarajio ya vijana hao.

“Ni matarajio yangu kwamba Mkutano huu utajitahidi kupanga malengo kufikia ajenda hiyo ya rasilimali watu na wito wangu kwetu sote pamoja na Washirika wetu wa Maendeleo ni kuhamasisha rasilimali kwa ajili ya uwekezaji katika kujifunza, afya, lishe, maendeleo jumuishi na ulinzi wa kijamii”, amefafanua Dkt. Mpango.

Kutokana na hayo Dkt. Mpango ametoa rai kwa wataalam wote waliohudhuria mkutano huo, kuja na sera za ubunifu ambazo zitaboresha matokeo ya mtaji wa rasilimali watu kwa Afrika kwa kuzingatia idadi kubwa ya vijana, pia ameshauri Taasisi za Fedha za kikanda kujitahidi kupata ufumbuzi wa changamoto za kifedha ili kuunga mkono msukumo wa Afrika wa kuharakisha maendeleo ya mtaji wa rasilimali watu. 

Vilevile, ameshauri  mkutano huo kujadili jinsi sekta binafsi inavyoweza kuhamasishwa kushirikiana kikamilifu na serikali kama wadhamini na wazalishaji wa mtaji bora wa rasilimali watu, pia taasisi za mafunzo za kiafrika ambazo ni nguzo muhimu katika uendelezaji mtaji wa rasilimali watu zinaweza na zinapaswa kusaidia Bara la Afrika kuimarisha uwezo wa ndani kusimamia na kutumia vyema rasilimali zilizopo.

Previous articleSIWANI, MBUNGE ASIYEFANYAKAZI HAFAI KUWA KIONGOZI – MTEMVU
Next articleWAZIRI MKUU AWASILI ST. PETERSBURG NCHINI URUSI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here