Na. Beatrice Sanga-MAELEZO
Serikali imesema kuwa itaendelea kukaribisha wawekezaji na kuweka mazingira rafiki ili kuwavutia zaidi wawekezaji wengi katika nyanja mbalimbali jambo litakalochangia kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla.
Hayo yameelezwa July 17, 2023 katika kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JINCC) jijini Dar es Salaam na Gilead Teri, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) wakati wa Mkutano uliondaliwa na Kituo hicho, Ofisi ya Msajili wa Hazina na Wahariri na waandishi wa habari wenye malengo ya kuelezea mafanikio na jitihada mbalimbali zinazofanywa na kituo hicho katika shughuli za uwekezaji nchini.
Teri amesema uwekezaji ni nyenzo muhimu kwa ukuaji wa uchumi nchini kwa maendeleo ya sasa na vizazi vijavyo, hivyo kituo hicho hakina budi kuhakikisha wawekezaji wanazidi kumiminika kwaajili ya shughuli za uwekezaji na biashara na kwamba kituo hicho kina mpango wa kuvutia uwekezaji wa dola bilioni 2 za kimarekani ndani ya miaka mitatu ijayo ikiwa ni pamoja na Sekta za kawaida na Sekta Mpya.
âMajukumu ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania ni pamoja na kuwafikia na kutoa chachu ya uwekezaji kwa wawekezaji wazawa na wageni, kuvutia uwekezaji kwenye fursa za uwekezaji nchini na kuweka mazingira Rafiki ya uwekezaji, ongezeko la watanzania katika miradi ambayo tunaisajili katika Kituo cha Uwekezaji ni kubwa, kwahiyo kuna muamko wa watanzania kuingia ubia, kuna muamko wa watanzania kusajili miradi mipya lakini pia kuna ongezeko na muamko mkubwa wa miradi ya wawekezaji kutoka nje.â Ameeleza Teri.
Teri amesema kuwa, kwa kipindi cha kuanzia January 2021 mpaka Juni mwaka huu Kituo cha Uwekezaji kimesajili jumla ya miradi ya uwekezaji na maendeleo 778, ambapo inatajwa kuwa imesaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa kutengeneza zaidi ya ajira mpya 125,382.
âThamani ya miradi hiyo ni dola za kimarekani Milioni 10,532, serikali imeongeza wigo wa mapato kwa miradi hiyo kusajaliwa, lakini pia miradi hiyo imeleta teknolojia mpya kutoka mataifa mengine (Transfer of Technology),â amefafanua Teri.
Teri amesema kuwa kituo hicho kitaendelea kuwasaidia wawekezaji baada ya kuwekeza ili wasipate changamoto za aina yoyote kupitia huduma kwa wateja (Aftercare Services), ambapo kwa sasa Kituo hicho kimeanzisha utaratibu wa kukutana na sekta mbalimbali pamoja na wawekezaji ili kujua changamoto ambazo wanazo na kwa namna gani wanaweza kuishauri serikali namna ya kuboresha mazingira ya uwekezaji.
Aidha, ameongeza kuwa kwa sasa kituo hicho kimeendelea kuvutia wawekezaji kwenye sekta ya sukari ili kumaliza changamoto hiyo, na pia kuuza nje ya nchi kutokana na kwamba Tanzania ina ardhi ya kutosha kuwekeza katika kilimo hicho.
âTunataka kufikia 2024 tusiwe na akisi ya sukari nchini, tunategemea kwa uwekezaji tuliokwisha kuvutia hadi sasa kuanzia mwisho wa mwakani Tanzania hatutokuwa na mahitaji ya sukari kutokea nje, tutakuwa na ziada ya sukari ambayo tutaweza kuiuza nje ya nchi.â
Kwa upande wake Angela Kilimali, Mhariri na Mwanachama wa Jukwaa la wahariri (TEF) amesema kuna haja ya waandishi wa habari kutangaza fursa mbalimbali zilizopo nchini ili kuhakikisha kwamba rasilimali iliyopo nchini inaendelezwa na kutumika kwa manufaa ya wengi ili kuondokana na umaskini unaowaombuka watanzania.
âSisi Wahariri tunafurahi kukutana na hizi Taasisi ambazo ziko chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kama ambavyo unafahamu kwamba watanzania wengi hawafahamu nini kipo ndani ya Serikali yao kwahiyo lengo la kukutana sisi kama wahariri tutahakikisha kwamba tunafuatilia kufahamu nini wanachokifanya lakini pia malengo ya Serikali ni yapi kuhakikisha tunasaidia kutangaza na wananchi kufahamu, tutakapozijua fursa kama Wahariri itakuwa ni rahisi kwa vyombo vyetu vya habari kuweza kuzitangaza kwa kushirikiana na hizi Taasisi mbalimbali na kuwafikia wananchi.â Ameongeza Kilimali.
Kituo cha Uwekezaji kimeendelea kuongeza jitihada za kuvutia uwekezaji hapa nchini kwa kufuatilia na kutembelea miradi kwa kufungua ofisi mbalimbali za kanda ambazo zimekuwa zikisaidia katika kutatua migogoro ya wawekezaji, lakini pia kituo hicho kimeendelea kuwashawishi wawekezaji wazawa kwa kuwaelimisha juu ya faida za kujiunga na huduma za kituo pamoja na kushiriki makongamano mbalimbali ya uchumi na uwekezaji ya ndani na nje ili kuvutia wawekezaji.
Mwisho