Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amewataka Watanzania kutumia fursa za lugha ya Kiswahili ili kuongeza kipato na kukuza uchumi wa taifa.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo Julai 6, 2023 wakati akizindua maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani ambayo yatafanyika kitaifa Julai 7, 2023 Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar.
Amesema kuwa lugha ya Kiswahili ina fursa nyingi kiuchumi na kuwataka Watanzania wakiwemo wanafunzi kuisoma na kuandika ili kutumia fursa zote muhimu za lugha hiyo duniani.
Waziri Mkuu amewahimiza Watanzania kutumia vizuri fursa ya kufundisha Kiswahili nchi mbalimbali duniani ambapo hadi sasa, wanahitajika Walimu 2800 katika nchi ya Afrika Kusini, Zimbabwe, Namibia, Sudani ya Kusini na Burundi.
Ili kufanikisha fursa hiyo, Serikali imeandaa mpango kazi wa pamoja wa kukuza na kubidhaisha lugha hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa kubidhaisha Kiswahili wa miaka 10 kuanzia mwaka 2022-2032.
Akimkaribisha mgeni rasmi kuhutubia hadhira hiyo, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Tabiia Maulid Mwita amesema kuwa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala ya mwaka 2020-2025 ambayo inasisitiza kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili.
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya pili ya Siku ya Kiswahili Duniani ya mwaka huu ni “Kiswahili Chetu, Umoja Wetu”, kwa mara ya kwanza yalifanyika mwaka 2022 baada ya kutangazwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) Novemba 23, 2021.